Wafanyabiashara waonywa udanganyifu uingizaji wa bidhaa
WAFANYABIASHARA na waingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi wametakiwa kuacha udanganyifu wanapoziagiza bidhaa zao nje ya nchi, kwani kwa kufanya hivyo watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Mkurugenzi Mkuu kutoka Tume ya Ushindani ( FCC), William Erio ameonya tabia hiyo katika kikao alichokutana na wafanyabiashara na waingizaji bidhaa kutoka nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Erio amesema kumekuwa na tabia ya udanganyifu miongoni mwa wajenzi ambao huagiza bidhaa zao nje, wasafirishaji wakubwa pamoja na wenye viwanda ambao hununua vitendea kazi kwa ajili ya wafanyakazi wao, ambao huagiza idadi kubwa ya vitendea kazi kuliko uhalisia uliopo.
” Mnapewa miradi lakini mnapoagiza vifaa mnasema ni matumizi binafsi. Unakuta kiwanda kina watu 40, unaagiza jozi 2000 hivyo kila mfanyakazi atavaa jozi 50 ni jambo ambalo halitawwzekana.
” Kuna kampuni ya uchukuzi wanaleta spea kila mwezi au baada ya miezi miwili jambo ambalo haliwezekani kila mwezi unabadili spea. Kama chombo cha serikali hatuwezi kuruhusu hilo,” amesema.
Amesema watu wamekuwa wakikalamika kuwa wana wacheleweshea biashata zao lakini wanapaswa kuingiza nchini vitu vyenye uhalisia.
Pia amesema ipo sheria ambayo inataka bidhaa inayoingizwa nchini ijulikane inatoka nchi gani, malengo yakiwa ni kuonyesha chanzo chake ni kipi ili ili kama kuna tatizo sheria ichukuliwe.
” Vilevike inawezesha bidhaa ile inapokuwa na tatizo unairudisha kule ilipotoka kama sheria inavyosema. Sasa kama bidhaa ile haijulikani inatoka nchi gani, kama haikuandikwa nchi yake unairudisha wapi wakati haina alama yoyote,”? amehoji.
Amesema hayo ndiyo matakwa ya kisheria hivyo wanapotaka kukagua bidhaa hizo wanafanya hivyo.
Awali amesema nia ya serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara katika maxingira mazuri ili wananchi wanufaike na bidhaa zao, uchumi wa nchi ukue.
Mfanyabiashara kutoka kampuni ya Estam Construction, Raya Eiriyamy amesema wamekuwa na changamoto wanapoagiza bidhaa kutoka Ulaya, inakuja nchini ikiwa imezalishwa China, na kuomba sheria za kimataifa ziwe wazi katika hilo.