Wafanyakazi MSF wauwawa DRC

DR CONGO : SHIRIKA la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limethibitisha kutokea kwa mauaji ya wafanyakazi wake wawili katika mji wa Masisi ulipo katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mfanyakazi mmoja alipigwa risasi na kujeruhiwa katika mazingira yanayohusiana na mizozo ya kikabila, wakati mwingine aliuawa katika mapigano kati ya waasi wa M23 na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka MSF, timu zao zimekuwa katika hatari mara kumi na tano tangu mwezi Januari mwaka huu, kutokana na machafuko yanayoendelea.
Hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa huku mapigano yaliposhika kasi kufuatia mashambulizi mapya kutoka kwa kundi la M23, yakiwa yameathiri pakubwa usalama wa raia na wafanyakazi wa misaada.
Emmanuel Lampaert, ambaye ni mwakilishi wa MSF kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameeleza kwa masikitiko mkubwa kwamba hali ya usalama katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ni mbaya sana.
Vituo vya afya na misaada ya kibinadamu vimekuwa vikikabiliwa na changamoto kubwa, huku waasi wakiendelea kukiuka haki za binadamu katika eneo hilo.
Shirika hilo limeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda wafanyakazi wao ili waweze kufanikisha kazi zao za kutoa msaada kwa wahanga wa vita na machafuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hali hii inatukumbusha umuhimu wa usalama katika maeneo yanayokumbwa na mizozo, ili kuweza kuokoa maisha ya watu wengi. SOMA: Mazungumzo ya Luanda yazae matunda amani DRC



