Wafanyakazi walalamika kuzuiliwa kuingia ofisini

DAR ES SALAAM: ZAIDI ya wafanyakazi 20 wa Hoteli ya Lark, iliyopo jijini Dar es Salaam, wamezuiliwa kuingia ndani ya jengo hilo siku ya mbili mfululizo bila kupewa taarifa rasmi, hali iliyozua taharuki miongoni mwao huku wakilalamikia hatua hiyo kuwa batili na ya kibabe.
Hoteli hiyo inayopatikana ndani ya jengo la Noble Center,Kampuni ya CRJE Investment (E.A) Ltd, imejikuta katikati ya mgogoro na mteja wao, Lark Hotel, hali iliyowalazimu wafanyakazi kushindwa kuendelea na majukumu yao licha ya kuwa na mikataba halali ya ajira.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake mbele ya waandishi wa habari, Dar es Salaam jana Mei 20,20, kiongozi wa wafanyakazi hao, Irene Mushi alisema kuwa tangu juzi wamezuiwa kuingia kazini bila maelezo yoyote kutoka kwa mwajiri wao.
“Siku zote tulikuwa tunafanya kazi kama kawaida, lakini kwa siku hizi mbili, tumejikuta milango ya maeneo muhimu ya hoteli kama vyumba vya kubadilishia nguo na mapumziko imefungwa na walinzi wa jengo. Pia mfanyakazi wa zamu ya usiku alizuiwa kuingia kazini bila sababu za msingi na alipohoji aliambiwa anatakiwa kuishia getini,” amesema Irene.
Ameongeza kuwa hatua hiyo imewaweka katika hali ngumu ya kimaisha kwani hawana taarifa yoyote rasmi ya kusimamishwa kazi, hivyo kushindwa kupanga maisha yao.
Kwa upande wake, mfanyakazi mwingine, Ester Besta amesema licha ya kuwa na mkataba halali wa ajira, amezuiwa kuingia kazini bila maelezo yoyote, na kwamba hata mwajiri wao hakuwapa taarifa kuhusu kufungwa kwa jengo hilo kwani endapo wangepokea taarifa hiyo wasingelalamika.
“Tuna familia zinazotutegemea. Hatujasimamishwa kazi na mwajiri wetu na hatujapewa taarifa yoyote, lakini tumefungiwa nje kama watovu wa nidhamu. Tunaomba serikali iingilie kati kututetea,” amesema Besta.
Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya Lark Hotel, Mwanasheria wa kampuni hiyo, Method Kagoma, amesema tayari wamefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, kupinga hatua zilizochukuliwa na CRJE dhidi ya hoteli hiyo.
“Tulipokea barua ya kutakiwa kuondoka ndani ya siku tatu, bila kufuata taratibu za kisheria. Tangu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, tayari kulikuwa na vitendo vya hujuma kama kukatwa kwa umeme ambavyo vilihatarisha shughuli za hoteli,” amesema Kagoma.
Ameeleza kuwa hatua ya CRJE kufunga milango ya jengo na kuwazuia wafanyakazi kuingia kazini bila amri ya mahakama ni kinyume cha sheria na ni uvunjifu wa mkataba baina ya pande hizo mbili.
“Kisheria, kama kuna mgogoro wa upangaji au madai ya kodi, kuna utaratibu maalum wa kisheria wa kufuata. Kufunga hoteli na kuwazuia wafanyakazi kufanya kazi bila amri ya mahakama ni ukiukaji mkubwa wa haki za wafanyakazi na makubaliano ya mkataba,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa Lark Hotel haijawasitisha kazi wafanyakazi wake, hivyo kuwazuia kufanya kazi ni sawa na kuingilia haki zao za msingi za ajira.
Kwa mujibu wa Kagoma, kesi hiyo tayari imewasilishwa mahakamani kwa njia ya mtandao na inasubiri kupangiwa tarehe rasmi ya kusikilizwa, huku akibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha haki inapatikana kwa pande zote husika, hasa kwa wafanyakazi walioko katika hali ya sintofahamu.
Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Kampuni ya CRJE ili kupata maelezo ya upande wao hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopokelewa.



