WAKULIMA wa zao la mpunga wamefurahishwa na kilimo shadidi chenye kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi ambacho kinapunguza gharama za uzalishaji huku tija ikiongezeka mara dufu ya kilimo cha kawaida.
Hilo limedhihirika katika kikao cha mwaka cha Wadau wa Kilimo Shadidi kilichofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Kituo cha Uyole mkoani Mbeya.
Mkulima Filbert Kadebe kutoka Skimu ya Mkula Wilaya ya kilombero amesema Kilimo cha kawaida alikuwa akipanda mbegu kilo 30 kwa ekari moja lakini kupitia kilimo shadidi anapanda mbegu kilo mbili hadi tatu kwa ekari.
Amesema hilo linawezekana kwa kutumia kitalu mkeka kinachosaidia kurahisisha hatua ya upandaji.
Vile vile amesema upandaji wa mche mmoja katika kilimo shadidi unatoa machipukizi mengi ambayo husababisha kuongezeka kwa mavuno ikilinganisha na kile cha kawaida.
“Kilimo Shadidi ni mchanganyiko wa teknolojia za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji kwa kubadilisha mfumo wa uratibu wa mimea, udongo, matumizi ya maji na virutubisho kwa lengo la kuongeza tija,”.
Naye Mtafiti Mkuu Kituo Cha Utafiti TARI Uyole Dk Atugutonza Bilaro amesema kilimo hicho kinatekelezwa Katika Halmashauri tano ambazo ni Kilombero, Chalinze, Iringa Vijijini, Mbarali na Bunda.
Dk Bilaro ambaye pia ni mratibu wa mradi amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wameweza kuwafikia wakulima 900 huku lengo kuu ikiwa ni kuwafikia Wakulima 4500 Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mradi.
Kwa upande wake kiongozi mwenza wa mradi kutoka taasisi ya utafiti ya Norway (NIBIO) Profesa Udaya Sekhar amesema lengo la kukutana ni kujadili maendeleo ya mradi, na kuweka mipango ya kutekeleza katika kipindi cha mwaka wa pili.
Mradi huo unatekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti ya Norway- na taasisi ya Utafiti ya Swamination nchini India .