Waganga wa jadi watwishwa lawama Geita

GEITA; JESHI la Polisi mkoani Geita limebaini baadhi ya waganga wa kienyeji na tiba mbadala wanatumia nafasi zao kufanya matukio ya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake kwa kisingizio cha matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo amesema hayo katika mkutano wa hadhara kijiji cha Nyakagomba wilayani Geita.

Kamanda Jongo amesema uchanguzi umebaini baadhi ya waganga wa tiba asili wanawalazimisha wateja wao wa kike kufanya mapenzi na kisha kuwarekodi picha chafu kama kitisho iwapo watatoa siri.

“Tutibu watu kulingana na vile mababu walituelekeza, sasa hivi imeingia tabia mbaya zaidi kwenu nyie waganga mnafanya zinaa na wake za watu kwa kuwadanganya mnawatibia.

“Mbaya zaidi mnaenda mbali mnawarekodi akitaka kukuacha unamtishia nitakuua, unaanza kumrushia zile picha ulizomrekodi na kumtishia kwamba utamdhalilisha,” amesema Kamanda Jongo.

Kamanda Jongo ametangaza vita kali dhidi ya waganga wa aina hiyo, kwani mbali na udhalilishaji pia wanachafua taswira ya waganga wa tiba ambayo imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa Afrika.

Pia amewaonya waganga wa tiba asili wenye tabia ya kupandikiza chuki na ramli chonganishi kwa wanasiasa kuacha mara moja, kwani wamekuwa chanzo cha matukio ya ukatili nyakati za uchaguzi.

“Changamoto kubwa tuliyonayo mnawadanganya sana wagombea, nyie waganga acheni, kutumia hizo mbinu kuwaharibu viongozi wetu, na hatimaye mnatusababishia uhalifu,” amesema.

Kamanda Jongo amewataka wananchi kutenga muda wao kusikiliza na kuchuja sera za viongozi kuelekea uchaguzi huo na kuwekeza katika kutunza maneno ya kisiasa kichwani badala ya kubaki nayo moyoni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button