Wageni wavuna fedha za miradi kuliko wazawa

DODOMA: SERIKALI imesema asilimia kubwa ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inawanufaisha wageni kutoka nje ya nchi kuliko wazawa.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema bungeni Dodoma kuwa sababu kubwa inayochangia hali hiyo ni uwezo mdogo wa makandarasi wa ndani wa kifedha, mitambo na wataalamu hivyo inakuwa vigumu kwao kushindana kwenye zabuni za kazi na makandarasi kutoka nje hasa kampuni za Kichina.

Bashungwa amesema hayo akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni Dodoma jana. Alisema kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Usajili wa Makandarasi, kati ya miradi 36,839, wazawa walitekeleza miradi 35,351 sawa na asilimia 95.9 ya miradi hiyo.

Advertisement

Hata hivyo, Bashungwa amesema miradi iliyotekelezwa na wazawa ni midogomidogo yenye thamani ya Sh trilioni 23.749, sawa na asilimia 38.5 ya thamani ya miradi yote iliyosajiliwa na kutekelezwa katika kipindi hicho ambayo ni Sh trilioni 61.638.

SOMA: Serikali: Wapinzani kaoneni miradi

“Hivyo, makandarasi wa nje ambao ni takribani asilimia 4.1 walitekeleza miradi michache yenye thamani kubwa (asilimia 61.5 ya thamani ya miradi yote),” amesema Bashungwa.

Kwa mujibu wake, kuna kampuni 14,800 za ndani za makandarasi, za ushauri wa wahandisi ni 252 na kampuni za wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ni 461.

Amesema kwa muda mrefu makandarasi na wahandisi washauri wa ndani wamekuwa na kilio cha ushiriki mdogo katika kazi kubwa za ujenzi.

Serikali: Wapinzani kaoneni miradi

“Sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa hali hiyo ni uwezo mdogo wa makandarasi hawa wa kifedha, mitambo na wataalamu ikilinganishwa na kampuni za nje,” ameeleza.

Ameongeza: “Wizara imedhamiria kuwawezesha makandarasi wazawa kushiriki kwenye kazi kubwa za ujenzi katika hatua na taratibu zote kuanzia mipango, usanifu, ununuzi, ujenzi, matengenezo, ukarabati na ubomoaji”.

Amesema kuwezesha wazawa kutaleta manufaa ikiwemo faida inayopatikana kutokana na utekelezaji wa miradi kubaki nchini na kutumika kukuza biashara za wazawa. Alitaja manufaa mengine ni kupunguza matumizi ya fedha za kigeni; kuongeza ajira na ujuzi kwa wataalamu wa ndani pamoja na kujenga uwezo wa kampuni za ndani kushindana kimataifa.

Bashungwa alisema aliunda timu ya wataalamu ichambue changamoto hizo na kuandaa mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ilitoa mapendekezo ikiwamo kurekebisha vipengele kwenye makabrasha ya zabuni ambavyo vina masharti magumu yanayosababisha wazawa washindwe kuvitimiza wakati wa kuomba zabuni na hivyo kuondolewa kwenye mchakato wa zabuni.