Wagombea wapishana fomu za ubunge

WAGOMBEA ubunge katika majimbo mbalimbali wamechukua fomu za kuomba uteuzi kugombea nafasi hiyo.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dk Doto Biteko alichukua fomu jana ya kuomba uteuzi agombee nafasi hiyo. 

Dk Biteko alihimiza wananchi wadumishe mshikamano na upendo miongoni mwao na wachague viongozi bora.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mtumba na Dodoma Mjini, Cosmas Nsemwa alisema hadi jana wagombea 16 kwa Jimbo la Mtumba na 14 wa Jimbo la Dodoma mjini walikuwa wamechukua fomu za kuomba uteuzi.

Alivitaja vyama kwa upande wa Jimbo la Mtumba ni AAFP, UPDP, Ada-Tadea, Sauti ya Umma (SAU), DP, NLD, Chama cha MAKINI, CCK, Tanzania Labour Party (TLP), UDP, Chama cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo, NRA, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia, kwa upande wa Jimbo la Dodoma Mjini ni UPDP, AAFP, ADA- Tadea, SAU, NLD, Chama cha MAKINI, CUF, UMD, DP, CCK, TLP, ADC, CCM na CHAUMMA.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Wilaya ya Bunda, Antonia Ndawi alisema wagombea saba kutoka vyama vya siasa wamechukua fomu za kugombea nafasi hiyo.

“Mpaka sasa, vyama vya siasa vilivyowasilisha majina ya wagombea wake na kuchukua fomu ni pamoja na ACT Wazalendo, CHAUMMA, CUF, NLD, NFP, NFDP pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema Ndawi.

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya alisema uteuzi wake ni heshima kubwa na ameupokea kwa moyo wa shukurani.

“Nimekuwa mwenye bahati sana, tulikuwa wengi tuliotia nia lakini baada ya mchujo na vikao vya chama niliibuka mshindi na nikateuliwa rasmi kuwa mgombea. Nawaahidi wananchi kuwa sitawaangusha,” alisema Bulaya.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Enock Koola alisema: “Mimi na wagombea ubunge wenzangu, pamoja na wale wanaowania nafasi za udiwani kupitia chama chetu ni kweli tuna uhitaji wa kuwahudumia wananchi ila kazi yetu itakuwa rahisi na nyepesi ikiwa tutaenda na Mama Samia”.

Mgombea wa Jimbo la Moshi Vijijini, Moris Makoi alisema akishinda ubunge atahakikisha wananchi wanapata huduma muhimu zikiwemo za afya, elimu na maji safi na salama.

Kwa upande wake, mgombea wa ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya CCM, Ibrahim Shayo alisema kipaumbele chake kitakuwa ni kuhakikisha kunakuwepo mshikamano miongoni mwa wananchi kwenye jimbo hilo.

Mgombea ubunge Jimbo la Bariadi Vijijini kupitia CCM, Masanja Kadogosa alichukua fomu katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.

Kadogosa alisema aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kumuunga mkono katika kuhakikisha anakwenda kuwatumikia kupitia nafasi hiyo.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Namtumbo, Juma Homera alisema anagombea ili awatumikie wananchi na kubadilisha wilaya hiyo.

 

Mgombea ubunge wa Jimbo la Longido, Dk Steven Kiruswa alisema iwapo atachaguliwa tena atahakikisha kila kata inakuwa maji ya uhakika, afya, barabara nzuri na mawasiliano.

Mgombea ubunge Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Isack Copriano alisema ameupokea uteuzi huo kwa moyo mkunjufu na ataendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kura za ubunge na za Rais zinapatikana kwa wingi jimboni humo.

Imeandikwa na Anastazia Anyimike (Dodoma), Naziah Kombo (Bunda), Heckton Chuwa (Moshi), Derick Milton (Bariadi), Muhidin Amri (Namtumbo) na John Mhala (Longido).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button