Wagombea zingatieni ratiba za kampeni

DAR-ES-SALAAM : JESHI la Polisi nchini limetoa wito kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu kuzingatia muda na ratiba ya kampeni waliyopangiwa ili kuepuka mivutano,migogoro,migongano au uhalifu kutoa kwani haitasita kumchukulia hatua mtu yoyote kama sheria za nchi zinavyoelekeza.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi David Masime imesema kuwa jeshi la polisi iko tayari na imejiandaa ipasavyo kuhakikisha inaendelea kulinda usalama wakati wote wa kampeni na baada ya kampeni.
“Kesho Agosti 28,2025 kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) kampeni za wagombea wa udiwani ,ubunge na urais zitaanza rasmi na jeshi la polisi linapenda kuwajulisha wananchi na wadau wote kwamba liko tayari na limejiandaa kuhakikisha tunaendelea kuimarisha usalama wakati wote,”ilisema taarifa hiyo.
Aidha jeshi limetoa wito kwa wagombea na wafuasi wao na wananchi wote kwa ujumla kukumbuka kuwa jukumu la kulinda amani, Utulivu na usalama ni la kila mwananchi wa Tanzania. SOMA:“Epukeni kampeni za matusi”
“Kamwe asiwepo mmoja wetu mwenye kukiuka sheria ,kanuni na taratibu wakati wote wa kampeni ni baada ya kampeni ili kuepuka vurugu au uhalifu wa aina yoyote kutokea,”alisisitiza taarifa hiyo.