Wahandisi wadhulumu zaidi ya Sh milioni saba za chakula

DAR ES SALAAM: MAMALISHE wa eneo la Msakuzi, Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Ritha Mrina amelalamika kudhulumiwa zaidi ya Sh milioni saba zilizotumika kuwalisha mafundi wanaojenga Shule ya Msingi Msakuzi.

Ritha ametoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo, Hashim Komba na watendaji wengine walipokuwa wanakagua ujenzi wa shule mpya ikiwa ni maandalizi ya kufungua shule Jumatatu ijayo.

Akiwa mbele ya mkuu huyo wa wilaya, baada ya kuruhusu wananchi kutoa malalamiko yao, amesema wahandisi wa mradi huo walimweleza awapikie chakula watamlipa jambo ambalo halikufanyika.

Advertisement

“Injinia Miraji, Injinia Salu, Mtei na Mussa wamekuwa wakila kwa maelezo pesa zikitoka watamlipa. Jambo ambalo halijafanyika.

“Pia mafundi walikula na pesa zao zilikatwa ili nilipwe jambo ambalo halikufanyika. Naomba mkuu unisaidie hili watoto wanakwenda shule ” alisema.

Naye mfanyabiashara wa vinywaji katika eneo hilo, Ester Omary amesema  naye anadai Sh 176,000 ambazo wahandisi hao walikunywa vinywaji.

Mkuu wa Wilaya Komba aliagiza Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), kuwakamata wahandisi hao na kuzilipa pesa hizo mara moja.