Wahandisi wafundishwa kujiajiri wenyewe

VIJANA wahandisi 123 waliosajiliwa na Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB)  wamepewa mafunzo ya ujasiliamari na ubunifu wa kibiashara  ili waweze kujiajiri wenyewe kwa kufungua makampuni yao binafsi ya ujenzi na shughuli nyingine mbalimbali kulingana na kozi walizosoma badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.

Seris Foundation ndiyo iliyoandaa mafunzo hayo ya siku nne ambapo vijana hao waliwasilisha bunifu zao kwa wataalamu  wa kujenga uwezo kwa wabunifu walioongozwa na Mkurugenzi Bunifu, Rhee Ji-Young.

Mkurugenzi Mtendaji wa Seris Foundation CPA Debora Wami amesema mafunzo hayo yamekuja baada ya vijana wengi wahandisi kukosa ajira tofauti na ilivyozoeleka zamani kwamba kila walipohitimu masomo yao walipata ajira za moja kwa moja kutoka serikalini ama makampuni binafsi.

Advertisement

Naye Mwenyekiti wa Seris Foundation Mhandisi Josephat Shehemba amesema kutokana na miradi bunifu mizuri iliyowasilishwa na wanafunzi hao watachuja na kupata mshindi mmoja atakayekwenda  kushindanishwa  kitaifa.

Msajili Msaidizi Mashirika yasiyo ya kiserikali, Mwanaisha Ali amewataka wahandisi hao watafute wafadhili na pia waombe mikopo ya asilimia 10 ili waweze kuendeleza bunifu zao kwa ajili ya atokeo chanya.

Nao Wahandisi David Ng’unda na Irene Makava wamepongeza mafunzo hayo huku wakiamini kwamba wanakwenda kufanyia kazi namna ya kuwasilisha na kuwafikia wanaowalenga ili waweze kunufaika na miradi yao.

Pia wahandisi hao wameonyesha hofu yao ya matumizi ya Akili Bandia (AI) kuchukua baadhi ya fursa na kuzifanyia kazi kwa mafanikio makubwa, hivyo wanashauri wenzao waongeze bidii katika bunifu ili waweze kupambana na Akili bandia katika fursa zilizopo.