Programu za ualimu wa amali kukabili uhaba wa walimu

MOROGORO: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimezindua programu mpya za Shahada ya Sayansi ya Ualimu katika mkondo wa Amali, hatua inayolenga kusaidia kutatua uhaba wa walimu wa masomo ya amali katika shule za sekondari nchini.

Programu hizo zitawaandaa walimu watakaofundisha masomo ya uzalishaji wa mazao, ufugaji, viumbe maji, bustani pamoja na nguo na mitindo, sambamba na kuwawezesha wahitimu kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje ya nchi pamoja na kujiajiri.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro, Rasi wa Ndaki ya Kilimo, Dk Nyambilila Amuri, amesema programu hizo zimeanzishwa kufuatia utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu ambayo imeanzisha mkondo wa amali katika baadhi ya shule za sekondari nchini.

Amesema programu hizo zinajumuisha Shahada za Ualimu katika Sayansi ya Uzalishaji wa Viumbe Maji, Uzalishaji wa Mazao, Uzalishaji wa Wanyama, Bustani pamoja na Nguo na Mitindo (Textile and Fashion).

“Kuanzishwa kwa programu hizi mpya kunadhihirisha dhamira ya chuo ya kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto za jamii kupitia elimu inayozingatia mahitaji ya dunia ya kazi,” amesema Dk Amuri.

Ameongeza kuwa programu hizo ni sehemu ya mkakati wa SUA wa kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kuajiriwa, kujiajiri, kusimamia miradi ya uzalishaji na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu.

Kwa mujibu wa Dk Amuri, mafunzo hayo yanaunganisha nadharia na vitendo kupitia mashamba darasa, maabara na maeneo mbalimbali ya uzalishaji, huku msisitizo mkubwa ukiwa kwenye mafunzo ya vitendo.

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzalishaji wa Mazao na Ualimu wa Amali, Atupakisye Mwasampeta, amesema alichagua kozi hiyo kutokana na kutambua nafasi kubwa ya kilimo katika uchumi wa Tanzania na maisha ya wananchi.

Amesema baada ya kuhitimu anatarajia kujiajiri katika sekta ya kilimo na, endapo atapata ajira ya ualimu, atatumia taaluma yake kuwasaidia wananchi kuongeza uzalishaji na maendeleo.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shahada ya Sayansi ya Uzalishaji wa Viumbe Maji na Ualimu wa Amali, Mudhihiri Ayub, amesema kozi hiyo ina fursa nyingi za ajira na kujiajiri ndani na nje ya nchi.

“Ninatarajia nikimaliza masomo nijiajiri katika ufugaji wa viumbe maji na kuwa mfugaji mkubwa ambaye pia atatoa ajira kwa wengine,” amesema Ayub.

SUA pia inasimamia Shule ya Sekondari Mafiga iliyopo Manispaa ya Morogoro, ambayo iliteuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufundisha masomo ya mkondo wa amali katika kilimo, ikiwemo uzalishaji wa mazao, bustani na mboga, uzalishaji wa wanyama pamoja na afya za mifugo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button