Katika mahafali ya 16 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa yaliyoongozwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Jakaya Kikwete leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Chuo hicho na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof William Anangisye, amewahimiza wahitimu kutumia elimu yao kama nyenzo ya kubuni ajira na kukabiliana na changamoto za maisha.
Profesa Anangisye alisema, “Dunia ya sasa inahitaji maarifa mapya na uthubutu wa kujifunza ili kuhimili ushindani katika soko la ajira kitaifa, kikanda, na kimataifa.”
Aliwahimiza wahitimu hao kuwa wabunifu, na iwafunze kujitegemea akisema; “Elimu yenu ni mtaji. Mnapaswa kuitumia kubuni fursa mpya za kiuchumi na kuimarisha maisha yenu.”
MAFANIKIO YA CHUO
Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Profesa Deogratias Rwehumbiza, alibainisha kuwa chuo kimepiga hatua kubwa kitaaluma kupitia ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi zaidi ya 10.
Ushirikiano huu umewezesha chuo kutambulika kimataifa, ikiwa ni pamoja na kupokea tuzo ya Taasisi Bora katika Elimu kutoka Business Executive Media Group. Tuzo hiyo ilitolewa katika mkutano wa African Academic Conference and Awards uliofanyika Novemba 24, mwaka huu, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Prof Rwehumbiza alisema mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya uongozi wa chuo na wadau mbalimbali.
Hata hivyo, alibainisha changamoto zinazokikabili chuo, ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kukamilisha kwa wakati miradi yake mbalimbali ya ujenzi.
“Tunaomba msaada zaidi wa kifedha kutoka kwa Mkuu wa Chuo, Dk. Jakaya Kikwete, ili kufanikisha ndoto za chuo,” alisema.
MAHITAJI YA MIUNDOMBINU BORA
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba ya wahitimu na Bulugu Batume, mhitimu bora wa mahafali hayo, wahitimu walitoa shukrani kwa juhudi za chuo kujenga mabweni mawili kwa fedha za ndani na bweni moja kupitia mradi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Hata hivyo, waliomba juhudi zaidi zifanyike ili kuboresha upatikanaji wa malazi kwa wanafunzi. “Tunatamani kila mwanafunzi awe na nafasi ya kukaa kwenye mabweni ya chuo ili kuboresha mazingira ya kujifunza,” alisema Batume.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Sinare Majaar, alisema mradi wa HEET ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotarajiwa kuboresha miundombinu ya chuo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hosteli za wanafunzi, maabara za fizikia, na majengo ya sayansi na midia anuwai.
TAKWIMU ZA MAHAFALI
Katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kikwete aliwatunuku digrii za awali wahitimu 1,562 ambao kati yao wanawake walikuwa 772 na wanaume 840.
Fani zilizotolewa ni pamoja na digrii ya elimu ya jamii (536), elimu katika elimu jamii (309), elimu katika sayansi (291), sayansi na ualimu (403), na sayansi katika kemia (23).
Aidha, wanafunzi 10, wakiwemo wanawake wanne, walihitimu na kutunukiwa digrii za uzamili.
Prof Anangisye aliwataka wahitimu kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa vitendo vyema na kushiriki kikamilifu kwenye jumuiya za wahitimu ili kusaidia maendeleo ya taasisi hiyo. ”
“Msiruhusu taswira ya chuo ichafuliwe. Endeleeni kuwa mfano bora kwa jamii na kushirikiana na chuo katika kujenga taifa letu,” alisema.
Mwisho