Wajasiriamali waingia kwenye mbio uchumi wa kijani

ARUSHA: Wafanyabiashara 20 wa Kitanzania wanaojihusisha na biashara zinazotoa suluhisho za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi wamejiunga na awamu ya tatu ya programu ya AfroGreen 3.0 inayolenga kuwawezesha kukuza biashara zao kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira nchini.

Programu hiyo yenye muda wa miezi tisa imezinduliwa na Westerwelle Startup Haus Arusha (WSHA) wakati wa maadhimisho ya miaka minne tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, ikiwa na msisitizo wa kuziandaa biashara changa kupata mitaji kupanua shughuli zake na kuongeza mchango wake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

AfroGreen 3.0 inafadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania kwa kushirikiana na Westerwelle Foundation ya Ujerumani.

Kati ya biashara 20 zilizochaguliwa, nane sawa na asilimia 40 zinaongozwa na wanawake, huku biashara 15 zikitoka Arusha na nyingine tano zikitoka Dar es Salaam na Iringa.

Akizungumza kuhusu programu hiyo Mkurugenzi wa Westerwelle Foundation Tanzania, Isaack Shayo, amesema tangu kuanzishwa kwa WSHA mwaka 2022 taasisi hiyo imekuwa ikitoa msaada kwa wajasiriamali wa Kitanzania kupitia kuwaunganisha na mitandao ya kimataifa na sasa inalenga kuwasaidia kupiga hatua zaidi kwa kuwaandaa kuvutia uwekezaji na kupata fursa za kibiashara.

Amesema mpango wa taasisi hiyo hadi mwaka 2030 umejikita katika kukidhi mahitaji mapya ya wajasiriamali, ikiwemo kuwaunganisha na wawekezaji fursa za kimataifa pamoja na kujenga ushirikiano na wafanyabiashara wenye uzoefu kwa ajili ya kupata ushauri na mitaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ajira na Kipato katika Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania Andrea Inglin amesema Serikali ya Uswisi imeendelea kuunga mkono programu hiyo kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wafanyabiashara kupata mitaji utaalamu wa kiufundi na mitandao ya kibiashara ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button