Wakili Ambindwile: Tujaze sanduku la kura kwa Samia na Mwinyi

IRINGA: Wakili maarufu na kada shupavu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Moses Ambindwile, ametoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kulinda demokrasia, kuheshimu katiba, na kuendeleza mapinduzi ya maendeleo yaliyoanzishwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi leo Oktoba 24, 2025 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar, mara baada ya mkutano mkubwa wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamebeba bendera za kijani na njano, Ambindwile alisema Tanzania ipo katika kipindi cha kihistoria cha ukuaji wa kiuchumi na kisiasa, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha safari hiyo haikatizwi.
“Ni wakati wetu wa kuonesha uzalendo kwa vitendo. Tujitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba, tupige kura za ushindi kwa Dk Samia Suluhu Hassan, Dk Hussein Mwinyi na wagombea wote wa CCM, kwa sababu wao ndio chaguo la maendeleo, umoja na ustawi wa Taifa letu,” alisema kwa msisitizo.

Ambindwile, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa, alitua Zanzibar tangu Oktoba 23 kuungana na makada wengine wa CCM katika kampeni za kuhakikisha chama hicho kinaendelea kuaminiwa na wananchi.
Akiwa amevalia shati la kijani, Ambindwile alihimiza Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano uliodumu kwa miongo mingi chini ya bendera ya CCM.
“Amani ni msingi wa maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote avuruge utulivu wetu. Tuchague viongozi wa CCM ambao wameonesha dira, uthubutu na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi,” alisema.
Aliwataka vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, akisisitiza kuwa sauti yao ina nguvu ya kulinda mustakabali wa Taifa.
“Uongozi wa Dkt. Samia umeonesha mwelekeo mpya wa mageuzi, hasa katika uchumi, elimu, afya, na uwezeshaji wa vijana na wanawake. Huu si muda wa kurudi nyuma — ni muda wa kuongeza kasi,” alisema.
Mkutano huo ulihudhuriwac na viongozi wakuu wa CCM, akiwemo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, na Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ambao kwa pamoja walitoa wito wa kudumisha amani na kujenga Tanzania inayojali maendeleo ya watu wake.



