Wakimbizi waaswa kurejea nyumbani misaada ikipungua

KIBONDO — Katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani leo Juni 20, 2025, viongozi wa wakimbizi na shirika la UNHCR wameitoa wito wa dhati kwa wakimbizi wa Burundi na maeneo mengine kuharakisha maamuzi ya kujiunga na mchakato wa kurejea nyumbani kwa hiari, huku wakionya kuwa misaada ya kibinadamu inazidi kupungua.
Samwel Kuyi, Mkuu wa Kambi ya Nduta, amesema licha ya changamoto za rasilimali na kushindwa kupata misaada kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wakimbizi wameendelea kuonyesha mshikamano na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.
“Miaka mingi tulikuwa tukipokea nguo mpya na misaada kwa siku hii, lakini mwaka huu tunasherehekea tukiwa kama tulivyo, na tunatambua kuwa wakati umefika wa kujiweka katika mwelekeo mpya,” alisema Kuyi.
Ameongeza kuwa mashirika makubwa ya misaada yanapanga kuondoka ifikapo mwisho wa mwaka huu, hivyo ni lazima wakimbizi watumie fursa ya kurejea nyumbani au kutafuta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo.
Henok Ochalla, Mkuu wa Ofisi ya UNHCR Kibondo, amepongeza Tanzania kwa ukarimu wake wa kipekee kwa wakimbizi, akisema kuwa ni nchi pekee Afrika iliyekuwa ikiwapokea na kuwaruhusu wakimbizi wa Burundi zaidi ya 162,000 kupata uraia tangu 1972.
Ameeleza kuwa zaidi ya wakimbizi 180,000 kutoka Burundi wamejiunga na mchakato wa kurejea nyumbani kwa hiari tangu mwaka 2017, na mchakato mpya wa “promotion” ya kurejea umeanzishwa mwaka huu na utaendelea hadi Desemba 2025. Mchakato wa tathmini za kinga na suluhisho unaendelea katika vituo vya kuondoka ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa usalama na haki.
View this post on Instagram
Ochalla alitoa ushuhuda wa usalama ulioimarika Burundi, akisema alipita kwenye maeneo kadhaa bila ulinzi wa polisi, jambo linaloonyesha hali ya amani inarudi. “Kama Burundi hainge kuwa salama, tungekuwa na walinzi wa polisi pamoja nasi,” alisema.
Maadhimisho hayo yamehusisha wadau mbalimbali wakuu wa misaada kama UNHCR, Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), World Vision, Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC), Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC), Medical Teams International (MTI) na Baraza la Wakimbizi la Denmark (DRC).
Viongozi hao wametoa wito kwa wakimbizi kutumia kipindi hiki cha nafasi kabla misaada ya misaada kukomeshwa, ili kupata suluhisho la kudumu na kurejea nyumbani kwa amani na heshima.