ZAIDI ya vikundi 40 vya wabanguaji na wakulima wa korosho mkoani Mtwara vitapatiwa elimu ya matumizi sahihi ya fedha ili kuwawezesha kutumia vyema mapato yao yanayotokana na zao hilo.
Hayo yamebainishwa wakati wa uzinduzi wa program ya “Anza Kutunza” inayoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali (FB EMPOWERMENT) linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani Mtwara.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa FB-Empowerment Fidea Bright amesema program hiyo imedhaminiwa na Benki ya NMB inayotekelezwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Oktoba 13, 2024 huku lengo likiwa ni pamoja na kuwaweza wabanguaji na wakulima hao ambao wengi wakiwa ni wanawake kutumia vyema mapato yao kwa matumizi sahihi na ya muda mrefu.
‘’FB-Empowerment imezindua rasmi program mpya ya ‘Anza Kutunza’ yenye lengo la kutoa elimu ya fedha kwa vikundi vya ubanguaji na wakulima wadogo wa korosho wengi wao wakiwa ni wanawake kuelekea msimu mpya wa korosho mwaka 2024/2025’’amesema Fidea.
Aidha vikundi hivyo vimetambulishwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii mkoani humo ambapo NMB kwa kushirikia na shirika hilo watahakikisha vikundi hivyo vinapata mafunzo thabiti ya matumizi sahihi hayo ya fedha kwani licha ya kuwa na matumizi sahihi na ya muda mrefu lakini waweze kukuza uchumi.
SOMA: Mambo yanoga ufunguzi msimu wa korosho
Amesema shirikia hilo linaunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza umuhimu wa kuwapatia wakulima wa mikoa ya kusini elimu ya fedha ili wanapopata mapato kutokana na mazao yao waweze kuyatumia kwa uangalifu na uwekezaji sahihi kwa manufaa ya muda mrefu.
‘’Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa CBT kwa kutufungulia milango ya kushirikiana na vikundi vya wakulima na kwa Nmb kuona umuhimu wa kuunga mkono uwekezaji huu pamoja na wadau wengine muhimu katika program hii ambao pia watashirikiana nasi katika kuhakikisha mafanikio ya program hii’’
Uzinduzi wa program hiyo umefanyika kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani na utaendelea hadi katika halmashauri ya mji Nanyamba mkoani humo kabla ya kuendelea maeneo mengine yenye vikundi vya wakulima wa korosho.