UNDP yanogesha ujasiriamali kwa vijana Dar

DAR ES SALAAM; Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kupitia Mpango wa Ubunifu wa FUNGUO, limehitimisha kwa mafanikio hafla ya utoaji wa Tuzo za YouthIgnite Awamu ya Tatu sambamba na kuzindua dirisha la tano la ufadhili wa kichocheo.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha ujasiriamali unaoongozwa na vijana pamoja na mifumo ya ubunifu katika vyuo vikuu nchini Tanzania.

Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo April 30, 2026, jumla ya biashara 20 zilizoanzishwa na wanafunzi zimetunukiwa kupitia mpango wa YouthIgnite Student Founders Fellowship na kufanya idadi ya biashara zilizoungwa mkono kufikia 60 tangu kuanza kwa awamu tatu za programu hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mradi wa Mpango wa FUNGUO, Joseph Manirakiza, amesema kuwa mpango huo utaendelea kuwezesha vijana kwa kuwekeza zaidi katika sekta za kilimo, ubunifu wa kidijitali pamoja na madini muhimu, ambazo ni nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP, John Lutere, amesema tangu kuanzishwa kwa mpango huo, FUNGUO imewekeza zaidi ya Sh bilioni 7.5 katika biashara changa bunifu 88, huku zaidi ya nusu ya biashara hizo zikifanikiwa kuvutia zaidi ya shilingi bilioni 18 kama mitaji ya ziada.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo umechangia kuzalisha na kudumisha zaidi ya ajira 10,000 nchini Tanzania, hatua inayodhihirisha mchango wa mpango huo katika kukuza uchumi jumuishi.
Kwa upande wa wadau wa maendeleo, Kiongozi wa Timu ya Ustawi Endelevu kutoka FCDO, Euan Davidson, amesema ushirikiano huo una lengo la kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Asilia kutoka Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Lamine Diallo, amesema uwekezaji katika sekta za kimkakati unasaidia kuimarisha uchumi na kuongeza ushindani wa biashara za ndani katika soko la kimataifa.



