Wakulima wa tumbaku kulipwa bil 13/- za mbolea ya ruzuku

TABORA – MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewahakikishia wakulima wa zao la tumbaku nchini kuwa watalipwa fedha zao za mbolea ya ruzuku walizoahidiwa na serikali za msimu uliopita kiasi cha Sh bilioni 13, mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Tabora pamoja na wakulima wa zao hilo katika viwanja Vya TBC mkoani Tabora jana, alisema serikali imeshatenga bajeti juu ya fedha hizo na tayari utaratibu wa kuanza malipo umefanyika na mwishoni mwa mwezi huu wakulima wote nchini watarejeshewa fedha zao.

Wakati huo huo, alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dk Khamis Mkanachi kuorodhesha kampuni zote za tumbaku zinazodaiwa na wakulima ili zifuatiliwe na hatua zichukuliwe. Alitoa kauli hiyo wakati alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwananchi Square wilayani Urambo.

Agizo hilo lilitolewa baada ya wakulima wa tumbaku wilayani humo akiwemo Anderson Kajuni kusimama na kuibua hoja kadhaa zikiwemo kutolipwa malipo ya mauzo yao kwa muda mrefu na wengine wakidai ruzuku waliyoahidiwa na serikali.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoani Tabora, Venance Msafiri alielezea mpango wa serikali katika kuzalisha tumbaku mkoani Tabora. Alisema wakulima wote wa Mkoa wa Tabora ambao wanadai fedha ya tumbaku watarejeshewa kwa haraka iwezekanavyo.

Nao wakulima wa zao hilo la tumbaku akiwemo Andrea Michael na Martha Donald waliishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo mwezi huu kwani itakuwa faraja kwa wakulima wa zao hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba alisema chama hicho kimeitisha bodi ya tumbaku nchini kusikiliza changamoto za wakulima na kufuatlia ruzuku ya wakulima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button