Wakutana Kagera kujadili fursa za maendeleo
BALOZI wa Tanzania nchini Rwanda, Richard Mutayoba na Balozi wa Rwanda hapa nchini, Charles Kalamba wamekutana kujadili wananchi wao wanavyoweza kunufaika na fursa mbalimbali za kimaendeleo na kiuchumi zilizomo maeneo yao.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika mkoani Kagera, Balozi Mutayoba alisema Tanzania na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri tangu zamani na zitaendelea kudumisha ushirikiano, huku akisisitiza kuwa ujio wa viongozi kutoka Rwanda kutaimarisha uhusiano wa kiuchumi na kindugu baina ya nchi hizo.
Ziara hiyo ambayo iliongozwa na viongozi mbalimbali na wafanyabiashara kutoka Jimbo la Mashariki nchini Rwanda, ilikuwa na lengo la kubainisha fursa zilizoko katika jimbo hilo linalopakana na Wilaya ya Ngara, Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera.
“Mkoa wa Kagera unazo fursa mbalimbali, lakini pia jimbo la Mashariki la Rwanda linazo fursa mbalimbali, hivyo basi kikao hiki kimedhamiria kuangazia maeneo mahususi, ambayo yataweza kuzinufaisha pande zote kiuchumi, “alisema Mutayoba.
Alisema nchi hizo kwa sasa zinashirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo usalama, biashara, elimu na afya, hivyo lazima waendelee kudumisha na kushirikiana katika masala mengine, ikiwemo nyanja za utalii, usafirishaji na kubadilishana uzoefu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albart Chalamila katika kikao hicho alisema serikali inaendelea kufungua nchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya zilizopo mipakani, ili kurahisisha shughuli za kibiashara.
“Leo hii ukienda pale Rusumo unaiona njaa ya kuboresha zaidi Rusumo ya Tanzania na Rusumo ya Rwanda ili paweze kukucha zaidi Katika mifumo ya kibiashara kwa watu wetu, Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameshatupatia fedha kwa ajili ya kujenga soko zuri la kimataifa pale litakalosaidia kuonesha bidhaa na biashara zetu,” alisema Chalamila
Gavana wa Jimbo la Mashariki la Rwanda, Gasana Emmanuel alisema kuwa serikali ya Rwanda na Tanzania zina lengo la kuboresha maisha ya wananchi wao.
“Serikali zetu zina lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora, lakini wananchi hawawezi kuwa bora bila kufanya kazi, hivyo basi nawaomba wananchi wetu kufanya kazi kwa bidii, lakini pia sekta binafsi na serikali kuja kwenye jimbo letu kufanya uwekezaji, tumeziona fursa zilizopo Kagera tunawashawishi wawekezaji wetu wazitumie vizuri muda wote tuko tayari, “alisema Emmanuel.



