Wakuu taasisi za umma wapewa maagizo tisa

SERIKALI imetoa maagizo tisa kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida ametoa maagizo hayo kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, wilayani Kibaha mkoani Pwani juzi.

Dk Kida alitoa maagizo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wapya 111.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi katika maeneo ya kazi. na aliwaagiza wazingatie sheria, kanuni na miongozo ya serikali na waendelee kujifunza ili kujenga uwezo wa taasisi za umma.

Dk Kida aliagiza viongozi hao wawe na usimamizi madhubuti wa rasilimaliwatu, rasilimalifedha na rasilimali nyingine za serikali zilizowekezwa katika taasisi.

“Lazima tuweke mbele maslahi mapana ya taifa katika kuziongoza taasisi ili serikali na nchi ifaidike na uwepo wa taasisi hizo,” alisema Dk Kida.

Aliwataka waimarishe ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuipunguzia mzigo serikali, wa kutafuta fedha za miradi mbalimbali.

Aliagiza watendaji hao waimarishe matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na wawezeshe mifumo isomane kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Kida aliagiza wajenge uhusiano imara wa kiutendaji baina yao na watumishi wanaowasimamia, bodi za wakurugenzi, wizara mama na wadau wengine.

Vilevile, aliwaelekeza watendaji hao waimarishe mifumo ya utoaji huduma na kujenga maadili mema mahala pa kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Programu ya mafunzo hayo ya siku tatu imeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya Uongozi kuwajengea uwezo watendaji wakuu wapya ili watekeleze majukumu kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Dk Kida aliwakumbusha watendaji hao kuwa taasisi na mashirika wanayoyaongoza ni mali ya umma hivyo umma unatarajia kuona matokeo chanya na yenye maslahi kwao.

Alisema programu ya mafunzo kwa watendaji walioteuliwa ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha watendaji wanafahamu wanatakiwa kufanya nini katika taasisi wanazozingoza.

Dk Kida alimpongeza Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu na timu yake kwa mageuzi yanayoendelea katika utendaji kazi wa taasisi za umma.

“Mageuzi yanayoendelea katika utendaji kazi wa taasisi na mashirika ya umma ni kielelezo tosha cha uongozi imara chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina,” alisema.

Dk Kida aliitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina iendelee na utaratibu huo ili kuzifanya taasisi za umma ziyafikie malengo ya serikali ya kuzianzisha taasisi hizo.

Alisema serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha taasisi na mashirika hayo yanakuwepo na kufanya kazi na kwamba ni nia ya serikali kuona taasisi hizo zinawajibika na kuwa na tija kwa jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button