Waliokufa ajalini Arusha kuzikwa Ijumaa

WATU watatu wa familia moja waliokufa baada ya gari yao aina ya Noah yenye namba za usajili 499 DMY kusombwa katika barabara ya Arusha-Moshi eneo la kata Amarura Tarafa ya King’oli wilayani Arumeru mkoani Arusha watazikwa Ijumaa katika makaburi ya familia yaliyopo eneo la Iboru.

Waliokufa katika ajali hiyo na wote wa familia moja ni pamoja na Angela Metili {26} ,Martha Metili {40}  na Lisa Metili {8} mwanafunzi wa shule ya Ilboru Arusha.

Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa familia ambaye aliomba kutotajwa jina alisema kuwa mwingine aliyekufa katika ajali hiyo aliyetambuliwa kwa jina la Brenda Amani(26) ambaye ni jirani wa familia ya Metili naye atazikwa siku hiyo hiyo.

” Kifupi wote waliokufa katika ajali hiyo wanazikwa Ijumaa Aprill 28 mwaka huu Ilboru ” alisema

Katika ajali hiyo dereva wa Noah alitambuliwa kwa jina la Neiman Metili(43) ambaye mke wake Martha alifariki yeye alinusurika toka akiwa mzima baada ya kufanikiwa kuchomoka katika usukani na kutelekeza gari lililosombwa na maji yaliyokuwa na kasi kubwa.

Katika ajali hiyo iliyotokea juzi majira ya saa 2.45 Asubuhi ,Mkuu wa Wilaya hiyo Emanuela Mtatifikolo alitoa pole kwa familia,ndugu na jamaa kwa kuwapoteza wanafamilia kwani msiba walioupata ni msiba mkubwa kwa wanafamilia ambao walikuwa wakienda katika mahafali ya kidatu cha sita Mkoani Kilimanjaro.

Mkuu huyo alisema maiti zote zilizopatikana katika ajali hiyo ziko katika hospital ya Wilaya ya Nnkoaranga Arumeru zikisubiri taratibu za mazishi nyumbani kwao Ilboru.

Mtatifikolo alitoa onyo kwa wakazi wa wilaya ya Arumeru kutodharau maji yanayopita barabara,mito na maeneo mengine kwani maji hayo huwa yana madhara makubwa kwa kuwa yanakuwa na kasi kubwa.

Alisema kuwa mvua kubwa inayonyesha katika Mkoa wa Arusha hususani katika wilaya ya Arumeru maji yake huvuka juu ya barabara ya Arusha –Moshi na maji hayo huwa yana kasi kubwa sana hivyo wenye vyombo vya usafiri wasiwe na haraka wasubiri hadi maji hayo yapungue.

Mkuu wa Wilaya alisema kuwa jeshi la zimamoto Mkoani Arusha linaendelea na jitihada za kusaka miili mingine amabyo haijapatikana katika ajali hiyo.

Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo walisema kuwa maji yalikuwa mengi yakipita juu ya barabara ya Arusha-Moshi na baadhi ya magari yalisimama kusubiri maji kupungua lakini dereva wa Noah alikaidi na kulazimisha.

Walisema vifo vya maji katika kipindi hiki huchangiwa na ukaidi wa madereva hivyo waliomba polisi kuwa macho kipindi mafuriko yanapotokea sehemu yoyote Arusha.

Habari Zifananazo

Back to top button