Waliomzushia kifo Dk Mpango kukiona!

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ametangaza nia ya Serikali kuchukua hatua za waliomzushia kifo Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango, ili kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao na kuwalinda wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa X, Disemba 10, 2023, Waziri huyo amesisitiza kwamba Serikali ina sheria zinazoelekeza matumizi sahihi ya mtandao pamoja na taasisi na watu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ili kulinda watumiaji mitandao na wananchi kwa ujumla.

Katika mahojiano aliyofanya na HabariLEO kwa njia ya simu, Waziri Nape amesema kuwa matumizi salama ya mtandao ni muhimu sana katika kuhakikisha amani na usalama wa nchi unakuwepo. Amesema zipo sababu za msingi na umuhimu wa matumizi salama ya mtandao kwa kuepuka matumizi mabaya kama ilivyotokea hivi karibuni kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kumzushia kifo Makamu wa Rais.

Akifafanua umuhimu wa kukuza amani na utulivu kwa nchi amesema “matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kusababisha taharuki na hata kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. Kutoa taarifa za uzushi wa kifo kwa wananchi kunaweza kuchochea hofu na wasiwasi kwa jamii.”

Amesema pia kuwa kulinda heshima za wananchi wote, matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kudhuru sana heshima na hadhi ya wananchi kwa ujumla. Amefafanua kuwa kutoa taarifa na kuzusha kuhusu kifo kwa mtu yeyote ni ukiukwaji wa heshima na utu wa mtu na inaweza kuathiri maisha yao na kuleta mtafaruku usio na sababu.

“Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanaweza kutumiwa kwa urahisi kutengeneza na kusambaza habari potofu na za uongo. Kumzushia mtu kifo ni mojawapo ya mbinu zinazoweza kutumika kudanganya umma na kusababisha machafuko. Tunalazimika kama Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaovunja sheria za matumizi salama ya mtandao. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kujenga jamii inayoheshimu mawasiliano na inayofanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo na amani ya nchi.” Amesema Nape.

Habari Zifananazo

Back to top button