WanaCCM Kata Arumeru warudisha vyakula, mali

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ambureni Jimbo la Meru Wilayani Arumeru mkoani Arusha ambao ni mabalozi wa nyumba kumi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kata wamerudisha katika ofisi ya chama kata hiyo vyakula na mali walivyopewa na mgombea udiwani wa kata kwa madai kuwa hiyo ni rushwa ambayo chama kinapinga mgombea kutoa katika kipindi cha uchaguzi.

Wanachama hao wamefikia uamuzi kurudisha ofisi Kata ya Ambureni baada ya mgombea huyo, Faraja Maliaki kugoma kufungua geti nyumbani kwake walipokwenda kupeleka vyakula kama mchele, mahindi, unga, sabuni, sukari na chumvi ili viongozi wa kata waweze kumkabidhi.

Mmoja wa wanaCCM aliyejitambulisha kwa jina la Eliaki Edward amesema viongozi wa chama ngazi za juu wamekuwa wakisisitiza wagombea kuacha kutoa rushwa kwa wajumbe wa kata na wilaya katika kipindi cha uchaguzi lakini wamekuwa wakipuuza maagizo hatua inayofanya wasiokuwa na fedha na mali kushindwa kupata uongozi na kuwapa mwanya wenye uwezo wa kifedha na mali kupita kwa ushawishi.

Edward amesema katika uchaguzi uliopita diwani anayemaliza muda wake ambaye amejitokeza tena kuwania nafasi hiyo alifanya hivyo hivyo na wanaCCM walilalamika kwa viongozi wa chama ngazi ya kata hadi wilaya lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Wanachama wengine waliojitambulisha kuwa Sabrina Ndosi, Mery Thadei na Loy Mbise wamesema kama mgombea anajua amefanya maendeleo katika miaka mitano iliyopita kitu gani kinasababisha atoe ushawishi wa vyakula na mali kwa mabalozi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kata na kwa nini asisubiri sanduku la kura katika uchaguzi wa ndani ya chama.

Katibu wa CCM Kata, Josiah Mollel alimekiri tukio hilo kutokea lakini amewaagiza mabalozi hao, wajumbe na wana CCM kupeleka vyakula na vifaa nyumbani kwa mgombea kwa kuwa chama hakijamtuma kufanya hivyo na kamwe chama hakiwezi kupokea vitu hivyo.

‘’Ni kweli niliwakuta ofisini na niliwakaribisha wakiwa na mchele, mahindi, unga, sabuni, sukari na chumvi lakini niliwaambia chama hakiwezi kupokea na niliwashauri kupeleka nyumbani kwa mgombea udiwani kwa chama hakijamtuma kufanya hivyo lakini wana CCM hao walisema kuwa nyumbani kwa mgombea kuna ulinzi mkali,’’amesema Mollel.

Akijibu tuhuma hizo, Diwani wa zamani ambaye anawania tena kiti hicho, Faraja Maliaki amesema waliofanya tukio hilo ni watu waliopangwa na wagombea wenzake wenye lengo la kumchafua kisiasa kwani yeye anajua taratibu na kanuni za chama na hajawahi kufanya hivyo pamoja na kwamba anamiliki taasisi ya Faraja Foundation inayotoa misaada mbalimbali katika kata hiyo na mara ya mwisho alitoa msaada wa mahindi na vyakula Disemba mwaka jana.

Katibu wa CCM Meru, Rehema Nzuye hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo la ugawaji vyakula na mali linalodaiwa kufanywa na Maliaki kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button