Wanafunzi Tulindane waishukuru serikali ujenzi maabara

BAADHI ya wanafunzi katika shule ya sekondari ya Tulindane iliyopo Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara wameishukuru serikali kwa kuendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea ikiwemo vyumba vya maabara vya kisasa.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo, baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Dairati Maulidi wa kidato cha kwanza shuleni hapo amesema kwa sasa wanajifunza kwa vitendo ikilinganishwa na hapo awali.
Uzinduzi wa shule hiyo umefanywa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Tax akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani humo lenye lengo la kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Mwanafunzi huyo amesema kabla ya ujenzi huo masomo ya sayansi walikuwa wakijifunza katika mazingira yasiyo kuwa rafiki kwasababu hawakuwa na vifaa vya kufanyia majaribio ya maabara hivyo wakijifunza kupitia kuangalia kwenye kitabu.
“Tunafurahi tumepata majengo mazuri yanayovutia na hasa hii maabara mwanzoni hatukuwa na vifaa vya kufanyia majaribio ya maabara ila sasa hivi tumepata vifaa tunashukuru sana”
Yasiri Saidi Mwanafunzi kutoka kidato hicho cha kwanza shuleni hapo, “Tunashukuru viongozi wetu kutuletea huu mradi wa shule ikiwemo vyumba vya maabara ya kujifunzia kwa vitendo”
Hata hivyo ameahidi kufanya vizuri katika masomo yao hasa hayo ya sayansi na kuleta ufaulu mzuri shuleni hapo.
Rukia Rashidi mmoja wa wazazi na mkazi wa mtaa wa Tulindane kwenye halmashauri hiyo, ameipongeza serikali kwa jitihada hizo kubwa za kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira mazuri.
Mkuu wa shule hiyo, Peter Mwalongo amesema ujenzi huo umegharimu Sh milioni 560 na matarajio yao watoto watakuwa wanafanya vizuri kwenye masomo yao.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri huyo wa ulinzi amesema atarajii kuona watoto wanakuwa watoro shuleni hapo na badala yake wafanye vizuri katika masomo.
”Natarajia ufaulu mzuri ili kutimiza ndoto zenu na hizi ndoto zitatimia kutoka kwao lakini kwa sisi wazazi wao kwa kuhakikisha kwamba kweli wanakwenda shule.