Wanahabari waanza kusajiliwa kidijiti, Tido aonya

MWENYEKITI wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Tido Mhando ameonya waandishi watakaojisajili kwenye mfumo kwa kutumia vyeti vya kughushi.

Tido alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa mfumo wa usajili wa waandishi wa habari (TAI Habari).

Alisema kumekuwa na taarifa zinazodokeza kuwepo kwa baadhi ya watu wanaojaribu kuwasilisha vyeti vya kughushi au nyaraka zisizo halali kwa lengo la kujipatia usajili na vitambulisho kinyume na taratibu.

Tido alisema kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya taaluma ya habari na pia ni kosa la jinai linalodhibitiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Waandishi wa habari watakaobainika kuwasilisha vyeti au nyaraka za kughushi watachukuliwa hatua kali bila kujali hatua waliokuwa wamefikia katika mchakato wa usajili,” alisema.

Tido alitaja baadhi ya hatua zitakazochukuliwa ni kufutiwa usajili wao, kuwasilishwa katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki na kupigwa marufuku kujihusisha na shughuli za uandishi wa habari au majukwaa mengine ya kitaaluma.

Alisema bodi hiyo itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiti na maombi yatafanyika kupitia mfumo wa TAI-Habari.

Tido alisema mahitaji wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo ni namba ya simu na barua pepe, picha ndogo, barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea, nakala ya kitambulisho cha taifa (NIDA) na ada ya ithibati Sh 50,000.

“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyo katika mfumo wa PDF na kuthibitishwa na mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET),” alisema.

Tido alisema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya uandishi wa habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.

Alisema kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ni hatua muhimu katika mchakato wa kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari kwa kuhakikisha wanahabari wanazingatia viwango vya juu vya weledi, maadili na uwajibikaji.

“Uandishi wa habari unapaswa kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii. Kupitia ithibati, waandishi wa habari wanapata utambulisho rasmi unaowawezesha kufanya kazi zao kwa heshima na uadilifu. Mbali na hayo, waandishi wa habari waliothibitishwa wanaweza kupata unafuu katika kupata habari kutoka kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kwa kuwa wanatambulika rasmi,” alisema Tido.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button