Wananchi wakumbushwa kufuatilia vitambulisho vya taifa

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amewaasa wananchi kufuatilia vitambulisho vyao vya Taifa mara baada ya kujisajili ili kuepuka changamoto mbalimbali zinazojitokeza wanapohitaji huduma muhimu za kijamii
Waziri Sillo ametoa wito huo alipofanya ziara ya kutembelea Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) sanjari na kufanya mazugumzo na watumishi wa Taasisi hiyo leo Januari 10, 2025 Dar es Salaam.

Naibu Waziri Sillo, ameeleza kuwa vitambulisho zaidi ya milioni 20 tayari vimetengenezwa na kupelekwa Ofisi husika lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kufuatilia vitambulisho hivyo kwa wakati.

Kadhalika Naibu Waziri alimpongeza Mkurugenzi wa NIDA na Watumishi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha huduma ya Vitambulisho inawafikia wananchi pamoja na ongezeko la uzalishaji wa vitambulisho hivyo
Aidha, Sillo alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya watu kujisajili zaidi ya mara moja hali ambayo husababisha usumbufu katika utunzaji na uandaaji wa taarifa za wananchi jambo ambalo linasababisha ugumu katika kuandaa taarifa za baadhi ya Wananchi wanaofanya hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) James Kaji amesema kuwa mamlaka hiyo imeanzisha mfumo wa kutuma jumbe za simu kwa wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho ambapo tangu walipoanza kutuma ujumbe wa simu ndani ya saa 24 pekee vitambulisho zaidi ya laki 400,000 vimechukuliwa na wahusika.

‘Natoa wito wale waliotimiza miaka 18 watumie mfumo wa mtandaoni kujisajili na kuwasilisha vielelezo vyao, ili inapotokea ajira ama kwenda chuoni, tuepuke ile mirundikano kwa wakati mmoja, na kupunguza changamoto ya utekelezaji wa jukumu’ Alisema Mkurugenzi huyo.

Alibainisha ili kurahisisha usajili wametoa namba kwa mtandao kukamilisha usajili, na wanapokwenda vituo vya mamlaka watatakiwa kwenda kwa ajili ya kupigwa picha na kupunguza mlolongo wa kukaa kwenye vituo muda mrefu.
Aidha kilio cha muda mrefu umepatiwa majibu kwa kukusanywa vitambulisho vyote vilivyokuwa kwenye ofisi za kata na kutumia mfumo kwa kutuma ujumbe kwa simu zao. ‘Waombaji mpaka Januari 31 ni matarajio yetu tutaweza kuwa tumetatua changamoto ya kuwapatia vitambulisho vile vilivyokwisha andaliwa na vinasubiri wahusika kuvichukuwa’ Alisema Mkurugenzi huyo.

Habari Zifananazo

Back to top button