Waonywa uchomaji moto Milima Uluguru

MOROGORO; Mhifadhi Mkuu wa hifadhi mazingira asilia Uluguru, Bernadetha Chile, amesema kuwa tabia ya wenyeji kuchoma moto katika Milima ya Uluguru ni hatari kwa mazingira na inachangia uharibifu mkubwa wa mfumo wa ikolojia.

Chile amesema hayo baada ya kukamilisha kazi ya uzimaji moto juzi Septemba 16, 2024 katika hifadhi asilia ya Uluguru, ambapo amewataka wananchi kuacha imani potofu ya kuangalia urefu wa maisha kwa kuchoma moto.

Advertisement

Amesema kuwa uchomaji moto huo unaofanywa na baadhi ya watu kwa ajili kupima urefu huo wa maisha,uwindaji wa ndezi pamoja na kusafisha mashamba unachangia uharibifu wa miti, ardhi, na viumbe hai vinavyotegemea mazingira hayo.

Amewataka wakulima kutambua umuhimu wa kulinda mazingira ikiwa ni pamoja na kutafuta njia mbadala za kupata mazao bila kuathiri mazingira, ambapo amesema uchomaji moto unachangia upotevu wa rutuba katika ardhi.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu ili kulinda rasilimali za asili na kuhimiza maendeleo endelevu katika eneo hilo

Amesema changamoto ya moto imekuwa ikiwasumbua karibu kila mwaka katika hifadhi hiyo , ambapo amesema kuwa kwa mwaka huu moto ulizuka Septemba 14 katika maeneo ya Bigwa Kisiwani, ambapo ulianzia mashambani na baadae kuingia hifadhini na walifanikiwa kuudhibiti.

Amesema Septemba 15, pia ulizuka katika maeneo ya mtaa wa uwalimu ambapo nao ulianzia katika mashamba na baadae kuingia hifadhini  kabla ya kuudhibiti.

Amesema juzi Septemba 16, walifanikiwa kuzima moto uliozuka katika mtaa wa Bong’ola na kwamba wakiwa katika harakati za kuzima moto wamegundua uwepo wa tanuri la mkaa na kueleza kuwa huenda ndiyo chanzo cha moto huo.

/* */