Wananchi watakiwa kuwapokea wawekezaji

KIGOMA: KIONGOZI wa Mbio za mwenge wa Uhuru, Ismail Ussi amewataka wananchi kuwapa ushirikiano wawekezaji wanaotekeleza miradi katika maeneo yao kwani miradi hiyo imekuwa na msaada mkubwa katika kuisaidia serikali kusogeza hudumwa kwa wananchi.
Ussi amesema hayo leo Septemba 20, wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Buha Energy kilichopo kijiji cha Kasange, Halmashauri ya Wilaya Kigoma kikiwa kituo pekee katika barabara ya Kigoma kuelekea Manyovu Wilaya ya Buhigwe mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Kiongozi huyo amesema kuwa taarifa alizonazo ni kwamba hakuna kituo chochote cha mafuta katika barabara hiyo ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 65 hivyo magari yote ni lazima yajaze mafuta Kigoma Mjini au Wilaya ya Buhigwe hivyo uwepo wa kituo hicho kumesogeza huduma karibu na wananchi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ussi (kushoto) akiwezindua kituo cha Mafuta cha Buha Energy katika kijiji cha Kasange Halmashauri ya Wilaya Kigoma (kulia) Mkuu wa Wilaya Kigoma, Rashid Chuachua.
Amesema serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na ndiyo wanawekeza kwenye maeneo mbalimbali hivyo wananchi nao hawana budi kushirikiana nao kwa kutoa au kuwauzia maeneo ya uwekezaji ili wafanye shughuli zao kwani ndani yake wananchi wananufaika kwa kupata ajira.
Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mwenge wa uhuru mwaka huu, Mkurugenzi wa Buha Energy, Justin Evarist amsema kuwa uwekezaji huo unafuatia fursa iliyopo na mazingirjia mazuri ya uwekezaji yanyojumuisha hali nzuri ya ulinzi na usalama inayoruhusu shughuli za uwekezaji na biashara kufanyika.
Kiongozi wa mwenge wa uhuru Ismail Ussi (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Buha Energy kilichopo kijiji cha Kasange Halmashauri ya Wilaya Kigoma wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea na kuzindua kituo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kigoma, Rashid Chuachua amesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi na ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi hivyo kutekelezwa kwa mradi huo kunasogeza huduma karibu ambayo imekuwa na mahitaji makubwa kwa vyombo vya usafiri vinavyotumia njia hiyo.