Wanaofuga wanyamapori majumbani wakemewe, wachukuliwe hatua

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi siku chache zilizopita alieleza kuuawa kwa fi si 17 baada ya kufanyika operesheni ya kuwatafuta wanyama hao ambao wamekuwa wakisumbua wananchi katika Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.

Jambo la kusikitisha wanyama hao si tu wanasumbua wananchi lakini wamesababisha madhara makubwa zaidi kwa kung’ata watoto na kuwaua.

Katika operesheni hiyo pia wamekamatwa baadhi ya wananchi ambao wamekutwa wanafuga wanyama hao majumbani kwao na mkuu wa mkoa ametoa onyo kwa wale wote ambao wanaishi na wanyama hao kinyume cha sheria.

Tunapenda kuanza kwa kumpongeza mkuu wa mkoa na timu yake kwa operesheni hii ya kuwasaka wanyama hao, sambamba na kuwachukulia hatua wale wanaowafuga kwa sababu zao mbalimbali ambazo kimsingi hazina faida yoyote zaidi ya kusababisha madhara kwa jamii.

Kinachoshangaza zaidi ni kuona fisi ambao mara kadhaa tumesikia wakishambulia watu, kutumiwa na wahusika kwa shughuli za usafiri.

Kwa akili za kibinadamu ni vitendo vya kustaajabisha na kuchafua taswira si tu ya Mkoa wa Simiyu lakini katika maeneo mengine pia yenye watu au jamii inayoamini kufuga fisi au wanyamapori bila kibali ni jambo la kawaida.

Tunaamini kuna kila sababu jamii si ya Itilima tu, nchi nzima kwenye watu wenye tabia ya kufanya matendo kama hayo kupewa elimu na mamlaka husika si za serikali tu bali kwa kushirikiana na wadau wakiwemo waganga wa tiba asili kama alivyoshauri mkuu huyo wa mkoa.

Jamii inapaswa kutambua na kuelewa kuwa fisi si chombo cha usafiri wala hana kazi nyingine yoyote katika maisha ya mwanadamu, bali ni mnyama ambaye anatakiwa kuishi porini au hifadhini na kinyume cha hapo ni kuvunja sheria.

Vitendo hivi pia vinatakiwa kukemewa vikali na kila mtu kwa sababu madhara yanayotokea ni makubwa zaidi kwani mbali na kujeruhi watu lakini wanyama hao wamekuwa wakisabisha vifo.

Jamii inapaswa kutambua mipaka yake na kuacha kufanya matendo ya ajabu kama haya ya kufuga wanyamapori
majumbani.

Wanyamapori wanapaswa kuishi porini hivyo kuwafuga nyumbani si salama kiafya kwa sababu hawapati kinga, hivyo ni rahisi pia kusababisha magonjwa kwa watu.

Matumaini yetu inapomalizika operesheni hii mkoani Simiyu kutakuwa safi na mikoa mingine nchini ambayo jamii
imekuwa ikifuga wanyamapori majumbani itakuwa imejifunza na kuelewa kuwa kufanya vitendo hivyo ni kinyume cha sheria za nchi na watakaoendelea kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button