Wanasheria wa ‘Mama Samia’ watoa suluhu migogoro 1505

Kampeni ya Kitaifa ya Msaada ya Kisheria ya Mama Samia imefanikiwa kutoa suluhu ya kudumu kwa takribani migogoro 1,505 kati ya migogoro 9,069 iliyoibuliwa tangu ilipoanza mwezi Machi 2023.
Aidha tangu kuanza kwa kampeni hiyo Jumla ya wananchi 779,191 wamenufaika na kupatiwa msaada wa kisheria ambapo kati yao wanawake ni 389,000 huku wanaume ni 396,000.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema hayo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo mkoani Geita.

Amesema mpaka sasa jumla ya mikoa 11 imeshafikiwa na kunufaika na kampeni hii na kwa awamu hii mbali na Geita pia mikoa ya Katavi, Tabora, Kigoma na Mtwara inaenda kunufaika na kufanya jumla ya mikoa 16.
Amesema dhamira kuu ya kampeni ni kutoa elimu ya sheria, kutoa msaada wa kisheria kwa waliokata tamaa, kutatua migogoro ya muda mrefu na kupanua uwigo wa haki kwa wasiomudu gharama.
Amesema wanasheria wa kampeni hiyo wakiwa mkoani humo watapita kwenye halmashauri zote sita, kata 60 (kata 10 kila halmashauri) pamoja na vijiji 180 kati ya vijiji 486 sawa na asilimia 37 ya vijiji vyote.

“Ipo migogoro ya aridhi, wananchi wetu wanapata shida, ipo migogoro kwenye sekta ya madini wananchi wanakuja ofisini kulalamika wamedhulumiwa, ipo migogoro ya mirathi, ipo migogoro ya ndoa.
“Zipo changamoto za ukatili, wa kijisnia na ukatili wa watoto, niombe sana wale wote mtakaojitokeza kuja kupata msaada wa kisheria, iwapo mambo yataenda mahakamani twende tukatoe ushahidi”, alisema.
Amewataka viongozi wa makundi yote ikiwemo viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, pamoja na waandishi wa habari kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.



