Wanasheria wa Samia watoa muongozo umiliki ardhi

TIMU ya wanasheria wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imewataka wananchi kuacha kuendekeza umiliki holela wa aridhi badala yake wafuate taratibu zote za kimila na kisheria kupata leseni.
Ofisa Maendeleo ya Aridhi na Makazi wilaya ya Bukombe, Augustino Simbaye amesema hayo kwa niaba ya timu wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namonge kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani hapa.
Simbaye amesema serikali inatambua aina kuu mbili za Hakimiliki ya aridhi ambazo ni Hakimiliki ya kimila na Hakimiliki ya serikali ambazo ni lazima kila mmiliki wa aridhi azingatie na kuheshimu muongozo wake.
“Mara nyingi tukinunua mashamba tunaandikishana, mtu anasema mimi nina hati pale, kumbe pale siyo hakimiliki yale ni maelewano kwamba pale umeuziwa kile kipande ni cha kwako.
“Hakimiliki ya kimila inatolewa na halmashauri husika, lakini kwa kushirikiana na halmashauri ya kijiji, na kwa utaratibu hatimiliki ya Kimila inatolewa kwa muda wa miaka 99 na ina sifa sawa na Hakimiliki ya serikali.
“Hakimiliki ya kimila unaweza kutumia kama dhamana ukienda kwenye taasisi za kifedha hizi unaweza ukakopesheka, kwa kutumia ile nyaraka uliyonayo ya Hakimiliki ya ya kimila”, amesema Simbaye.
Amesema hakimiliki za serikali zipo za aina tatu ambazo ni hakimiliki ya ofa, hakimiliki kubwa, kwa mashamba yaliyopimwa pamoja na leseni ya makazi ambayo hutolewa kwa watu waliojenga kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Amesema jambo la kuzingatia ni kwamba mtu anapomiliki aridhi raslimali zilizopo ikiwemo madini, gesi mafuta vyote vinamilikiwa na Jamuhuri, siyo mali ya mtu binafsi bali ni mali ya umma na mwenye dhamana yake ni Rais.
Amesema aridhi imegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza ni aridhi ya kijiji na mwenye mamlaka nayo ni serikali ya kijiji, baada ya hapo kuna aridhi ya hifadhi ikiwemo maeneo ya hifadhi za barabara.
“Kwa hiyo mtawala mkuu wa aridhi ni mheshimiwa Rais ndiye amekasimiwa mamlaka hayo, baada ya hapo kuna waziri wa aridhi, lakini baada ya hapo kuna Kamishina wa aridhi ambaye ndio Mtendaji Mkuu wa Aridhi”, amesema.
Mjumbe wa serikali kijiji cha Namonge, Mussa Malunde amekiri kuwa ipo changamoto kubwa ya migogoro ya aridhi hasa kwenye maeneo ya vijijini kutokana na ukosefu wa elimu ya hakimiliki kwa wananchi.
Naye Nkamba Burai ameishukuru Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafungua macho juu ya hatua za kufuata ili kupata hakimiliki ya kiwanja ama aridhi kwani wanawake wengi wananyanyasika.



