WANAWAKE na wasichana 25 kutoka mikoa mbalimbali wamefanyiwa upasuaji wa plastiki wa bure wa urekebishaji wa mwili katika awamu ya tisa ya program hiyo iliyofanyika kuanzia Novemba 29, Dar es Salaam.
Upasuaji huo uliofanywa na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kwa kushirikiana na Reconstruction Women International (RWI) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili utahitimishwa leo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mkuu wa Idara ya upasuaji wa Aga Khan Dk Athar Ali amesema wamefanikiwa kurejesha tabasamu kwa wanawake na wasichana waliokumbwa na ukakamavu, ulemavu wa kutembea, majeraha ya moto, ukatili wa kijinsia na ajali.
“Upasuaji huu umefanikiwa chini ya madaktari bingwa kutoka RWI, Marekani, Canada, Ulaya kwa kushirikiana na hospitali za Aga Khan, Muhimbili, Bugando, Mnazimmoja Zanzibar,” amesema na kuongeza kuwa tangu wameanza program hiyo mwaka 2016 wameshafanya upasuaji kwa zaidi ya wanawake na wasichana 300 hadi 2023.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili ambaye pia, ni kiongozi wa RWI kutoka Marekani Andrea Pusic amesema program hiyo imelenga kurejesha uwezo wa kimwili kwa wanawake na wasichana ambao wana mchango katika uchumi wa nchi na wamebeba majukumu ya kifamilia.
“Huu ni mwaka wa tisa wa ushirikiano wetu wenye mafanikio makubwa, tumekuwa na uwezo wa kuboresha uwezo wao wa kimwili na muonekano wao. Pia, tumekuwa tukitoa mafunzo kwa madaktari kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya upasuaji huu,”amesema.
Daktari bingwa wa upasuaji wa Aga Khan Aidan Njau amesema walianza kuchukua wagonjwa kutoka Dar es Salaam lakini kwa sasa wamechukua Tanzania nzima na kwamba walikuwa wakiangalia walioathirika kwa ukubwa.
Ametolea mfano kwa baadhi ya wanawake waliokutana nao waliotolewa matiti kutokana na saratani kwa hiyo wamewatengeneza na kuwaweka matiti bandia, pia kuna walioungua hadi viungo vikabaki kama vipapatio vya kuku wamerekebishwa kuwa vizuri.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk Edwin Mrema amesema wakati wanaanza hawakuwa na madaktari waliobobea katika upasuaji huo lakini kwa ushirikiano na serikali na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na wataalam na yale ya Chuo cha afya na Sayansi shirikishi cha Muhimbili kuna madaktari tisa na wengine wataendelea kuzalishwa kila mwaka.
Katika kuunga mkono juhudi hizo za upasuaji Pakistan Women Wing chini ya chama cha afya cha Pakistan kimechangia sh milioni 10.1.