Wanawake viongozi Afrika waweka nguvu ukatili wa kijinsia

Dar es Salaam: Katika juhudi za kuifanya Afrika kuwa salama kwa wanawake na watoto, wanawake viongozi kutoka zaidi ya nchi 16 barani wamekutana jijini Dar es Salaam kuunga mkono Makubaliano Mapya ya Umoja wa Afrika ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana (AU-CEVAWG).
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Felister Mdemu, akifungua kikao hicho cha viongozi wanawake wa Afrika leo Julai 21,2025 jijini Dar es Salaam, amesema Tanzania ipo mstari wa mbele katika mapambano haya kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ( MTAKUWA) , unaolenga kuleta usalama, amani na haki kwa wanawake na watoto.

“Zamani ukatili ulifichwa, lakini sasa jamii imeelimika, taarifa zinatolewa, na hatua zinachukuliwa. Haya ni mageuzi ya kweli,” amesema Mdemu.
Makubaliano hayo ya AU yaliyopitishwa Februari 2025 nchini Ethiopia, yanalenga kukomesha ukeketaji, ndoa za utotoni, na aina zote za unyanyasaji wa kijinsia, huku yakisisitiza huduma bora kwa waathirika na utekelezaji thabiti wa sheria.
Kwa upande wake, Moreen Onyango kutoka FEMNET amesema Afrika sasa ina mwongozo halisi wa pamoja kupinga ukatili wa kijinsia uliopitishwa na wakuu wa nchi katika Kikao cha 38 cha Umoja wa Afrika kilichofanyija Februari 2025 Addis Ababa Ethiopia.

Naye Cecilia Shirima wa Young and Alive , amesema mkutano huo unalenga kuhamasisha utekelezaji wa mkataba huu kwa kila nchi.
Baadhi ya nchi zilizoshiriki ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Congo, Botswana, Eswatini, Zimbabwe na Afrika Kusini.


