Wanawake waandika rekodi mpya uchaguzi 2025

DODOMA : KATIKA mbio za kuwania kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa Uchaguzi Mkuu 2025, taifa linashuhudia rekodi ya kisiasa ikiandikwa baada ya wanawake watatu kujitokeza kuwania urais na 10 wakiwa katika nafasi ya makamu wa rais. Kujitokeza kwa wanawake watatu kuwania kiti cha rais kunavunja rekodi na kuweka idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu kisiasa kufikia sita tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.
Waliowahi kuwania kiti cha rais ni Anna Senkoro kupitia PPT-Maendeleo mwaka 2005, Anna Mghwira kupitia ACT Wazalendo mwaka 2015 na Queen Sendiga kupitia Alliance for Democratic Change (ADC) mwaka 2020. Hata hivyo, kwa mwaka huu wanawake watatu wamejitokeza ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwajuma Milambo kutoka Union for Multiparty Democracy (UMD) na Saum Hussein Rashid kupitia United Democratic Party (UDP).
Pia kwa mara ya kwanza, vyama 10 kati ya 18 ambavyo vimechukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) vimetoa wanawake kama wagombea wenza. Hatua ya vyama vya siasa kusimamisha wanawake katika nafasi za juu za uongozi, ikiwemo urais na makamu wa rais, inaashiria kuimarika kwa ajenda ya usawa wa kijinsia katika siasa za Tanzania.
Akizungumza, Mwajuma alisema hatua ya UMD kuwasimamisha mgombea wa urais na mgombea mwenza wote wanawake ni sehemu ya mkakati wa kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi za maamuzi. “Katika kutafuta 50 kwa 50 kwenye ngazi za maamuzi, mlango wa kuingia ni vyama vya siasa. Hivyo, nikiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya UMD nimeona ni lazima nihakikishe usawa wa uongozi ndani ya chama.”
Alisema kwa chama hicho si tu kwenye mgombea urais na mgombea mwenza, bali ndani ya chama viongozi wa juu wa kitaifa kati ya 18, nafasi 12 ni za wanawake. “Kwa hiyo tunaitekeleza kwa vitendo Azimio la Beijing,” alisema Mwajuma. Kwa upande wa mgombea urais wa Alliance for African Farmers Party (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru alisema chama hicho kimetumia kigezo cha uzalendo kama msingi wa uteuzi wa mgombea mwanamke nafasi ya makamu wa rais.
“Kwao, kiongozi anayejali nchi yake ni rafiki wa kina mama, na hivyo masuala ya kijamii yenye kugusa familia yatawekwa mstari wa mbele,” alisema Kunje. Chama cha MAKINI, Mwenyekiti wake Coaster Kibonde alisema uteuzi wa mgombea mwanamke unatokana na imani kwamba wanawake wanaweza kufanya vizuri.SOMA: Chadema yaacha kuwahoji akina Mdee
Alitoa mfano wa Rais Samia kama uthibitisho hai wa uwezo wa mwanamke katika nafasi ya juu ya uongozi. Mgombea wa urais wa UDP, Doyo Hassan Doyo alisema chama kimemteua Chausiku Khatib Mohamed ili kufikia ajenda ya 50 kwa 50 na katiba ya chama inasisitiza hilo.
Mgombea urais wa Tanzania Labour Party (TLP), Yusta Rwamugira, alisema chama kimesimamisha Amana Suleiman Mzee kuwa mgombea mwenza kutoa fursa kwa wanawake. Mgombea urais kwa Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara alisema chama kimemteua mwanamke kwa kutambua wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
“Tumemteua Satia Mussa Mbebwa kuwa mgombea mwenza kwa kufahamu mchango wa wanawake katika maendeleo, hivyo tumeamua kuwa nao bega kwa bega.” Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salim Mwalimu alisema chama chao kimesimamisha mgombea mwanamke ambaye anabebwa na uwezo na utashi wake.
“Hata chama kiliponiambia una nani kama mgombea mwenza, wala sikusita kumchagua Devotha Minja. Sikumuangalia kama ni mwanamke bali nilimuangalia kuwa ni mtu ambaye falsafa zake, fikra zake, mitazamo yake na namna alivyoipigania nchi hii,” alisema.
Naye alikiri kuwa kumekuwa na mwamko wa wanawake kujitokeza kwenye udiwani, ubunge na hata mbio za urais na makamu wa rais. Mgombea urais wa National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), Haji Ambar Khamis, alisema chama kimemsimamisha Dk Eveline Munis ikiwa ni hatua ya kuifikia 50 kwa 50 usawa wa kijinsia. Mgombea urais kupitia UDP, Saum Rashid alisema.
“Tukiwa viongozi wanawake tunakwenda kutatua changamoto zinazowabagua wanawake katika sera na sheria ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote bila kujali jinsia.” Naye mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo alisema chama kimemsimamisha Husna Mohamed Abdallah ikiwa ni njia ya kuionesha jamii kuwa wanawake ni viongozi