MAWAKILI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) , wamedai hawana nia ya kuwahoji maswali ya dodoso Halima Mdee, Ester Matiko na Ester Bulaya juu ya kiapo kinzani walichowasilisha mahakamani hapo katika kesi waliyofungua kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.
Hatua hiyo imefikiwa leo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha katika Mahakama Kuu, Masijala Kuu, baada ya wakili wa Chadema, Hekima Mwasipo kuieleza mahakama kuwa wameamua kufunga maswali yao baada ya kutafakari kwa kina na kubaini kwamba hawana maswali ya ziada kwa wabunge hao.
Wabunge waliopo katika shauri hilo ni Halima Mdee, Grace Tendega, Nursat Hanje, Cecilia Pareso, Hawa Mwaifunga, Esther Matiko, Esther Bulaya, Jesca Kishoa, Felister Njau, Agnesta lambart, Asia Mohamed, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Styella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza na Naghenjwa Kaboyoka.
Awali wakili wa Serikali Jesca Shengena ,akisaidiana na Stanley Katokola alidai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa na wapo tayari, ambapo Mbunge Jesca Kishoa atamalizia kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa Chadema kuhusu malalamiko yake ya kufukuzwa uanachama kinyume cha sheria.
Hata hivyo wakili Mwasipo alidai kuwa upande wao wa wajibu maombi wamefunga kuuuliza maswali hayo. Kishoa alianza kuulizwa maswali hayo ya dodoso Novemba mwaka jana, huku akitanguliwa na Tendega, Hanje, Pareso na Mwaifunga ambao walihojiwa maswali hayo ya dodoso kuhusu hati zao za viapo.