Wapatiwa vifaa kufungiwa huduma ya maji
WANANCHI wa maeneo ya Kisanga, Kilimahewa, Muungano, Kinzudi, Majengo, Salasala, Muungano na Mivumoni waliokamilisha taratibu za kupata huduma ya maji wameanza kupatiwa vifaa kwa ajili ya kufungiwa huduma ya maji kwenye Mkoa wa kihuduma DAWASA Mivumoni.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa uboreshaji huduma ya maji kutoka Bagamoyo hadi Makongo unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2022.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema wakazi zaidi ya 90 wa maeneo hayo watanufaika na huduma hiyo yamaji safi.
Akizungumza leo Oktoba 19, 2022, Luhemeja amesema kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo na kutimiza maono ya Rais wa Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema dhumuni kubwa la mradi huo ni kuboresha huduma ya maji na kufikia wananchi kwa asilimia 95 kwa wateja wapya, ambao hawajawahi kupata huduma ya maji safi na salama hapo awali.