Wapigapicha chipukizi, wabobezi, jukwaa moja
*Ni katika maonesho ya Dar Foto Festival
DAR ES SALAAM: Wapiga picha 12 wa Tanzania, wanaofanya shughuli zao mtaani, wameteuliwa kushiriki maonesho ya picha ya Dar Foto Festival 2024.
Maonesho hayo yamezinduliwa leo katika jengo la Old Boma likiwa na kauli mbiu ya Watu, Uchumi, Mabadiliko.
Akizungumza na HabariLeo, Muandaaji wa maonesho hayo Andrew Manua amesema yatafanyika mwezi mzima kuanzia leo hadi Februari 29, 2024.
Amesema, mbali na maonesho pia kutakuwa na mada mbali mbali kutoka kwa wataalamu mashuhuri na wapiga picha chipukizi watapata wasaa wa kupewa ushauri na nyenzo mbali mbali kwa ajili ya kuboresha kazi zao.
Andrew amesema kuwa wameamua kuandaa maonesho hayo ili kutoa nafasi kwa ajili ya wapigapicha pekee wa hapa nchini waweze kutambulika kimataifa.
Amesema, maonesho hayo ni ya pili kufanyika nchini yakizaminiwa na Goethe-Institut na Dutch ambapo mwaka juzi yalishirikisha wasanii 20 kutoka nchi 15.
“Mwaka huu tumeamua kutoa ‘platform’ zaidi kwa watanzania, tuna wapigapicha wazuri huko mitaani lakini hakuna sehemu ambako wanaonyesha kazi zao, tofauti na wenzetu kama Afrika Kusini zipo sehemu nyingi sana za maonesho,”amesema Andrew
Kwa upande wa baadhi ya washiriki wakizungumza na Habari Leo wamesema kilichowasukuma kushiriki ni kuonyesha maisha halisi ya watanzania kupitia sanaa zao za picha.
Natalia Msungu anasema sanaa aliyoiwasilisha kwenye maoesho hayo inaonyesha pilika pilika za wakazi wa Dar es Salaam katika kujitafutia maisha na kujiinua kiuchumi.
“Tuna kitu cha tofauti tunaweza kufanya kwa Dar na kuonyesha wapiga picha wa mtaani wachukuliwe kwa ‘userious’ tuna vitu vingi ambavyo tunaweza kuvionyesha,”amesema.
Nae, Getrude Malizeni msanii wa sanaa za uoni upande wa kuchora, kupaka rangi na video, amesema kazi alizoziwasilisha zimejikita zaidi katika sanaa ya wanawake kwa ujumla kuonyesha kazi ambazo wanazifanya katika jamii na mchango wao,
“Picha zangu zinahusu harakati za Mama lishe, washona nguo, wasusi, wauza mboga mboga ambao ni watu wenye mchango mkubwa katika maisha yetu ya kila siku, katika familia zetu hazipiti siku mbili hatujatumia mboga mboga za majani lakini thamani zao hazichukuliwi, hivyo video inaonyesha hali zao halisi,”