Waraka waelekeza utekelezaji Sera ya Elimu

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Waraka wa Elimu Namba 01 wa Mwaka 2025 kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na mitaala iliyoboreshwa ya mwaka 2023.

Kamishna wa Elimu wa wizara hiyo, Dk Lyabwene Mtahabwa amesaini waraka huo Januari 10, mwaka huu na ulianza kutumika Januari 13, mwaka huu.

Waraka huo unahusu elimu ya awali, msingi na sekondari na kubainisha kuwa katika mitaala iliyoboreshwa kuna Elimu ya Jumla na Elimu ya Amali na kuwataka wakuu wa shule zilizoanza kutekeleza sera hiyo kuhusu elimu ya sekondari kwa mtaala ulioboreshwa, kuwajengea uelewa wanafunzi kuhusu elimu hiyo.

Waraka huo unaeleza kuwa wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaendelea na utekelezaji wa sera hiyo mpya na mitaala iliyoboreshwa.

Katika hilo utekelezaji wake ni awamu ya pili na umeanza Januari mwaka huu kwa ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari.

Waraka huo unaeleza kuwa kwa elimu ya awali wakuu wa shule na wadau wote wanaohusika na elimu wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza walioanza ngazi hiyo kwa mwaka 2024 wanaendelea na darasa la pili mwaka 2025.

Pia, wanafunzi wa darasa la pili wanaendelea na mtaala ulioboreshwa kwa darasa la tatu mwaka 2025 na wanafunzi wa darasa la tatu wanaendelea na mtaala ulioboreshwa kwa darasa la nne mwaka 2025.

Aidha, waraka huo unawataka wanafunzi wa darasa la V, VI na VII mwaka 2024 waendelee na mtaala uliokuwepo kabla ya maboresho ya mitaala ya mwaka 2023 hadi kuhitimu ngazi ya elimu ya msingi.

Kwa elimu ya sekondari, waraka huo unaeleza kuwa awamu ya kwanza ya utekelezaji ilianza mwaka 2024 kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopangiwa kusoma katika Mkondo wa Amali kwenye shule 39 kati ya hizo za serikali ni 25 na zisizo za serikali 14.

Waraka huo umewataka wanafunzi hao kuendelea na kidato cha pili mwaka 2025 kwa kutumia mtaala ulioboreshwa.

Kwa shule zote za sekondari ngazi ya chini kwa maana ya za serikali na zisizo za serikali zitaanza kutekeleza Mtaala Ulioboreshwa kidato cha kwanza Mkondo wa Elimu ya Jumla Januari mwaka huu.

Kadhalika, mtaala ulioboreshwa kidato cha kwanza Mkondo wa Amali utatekelezwa katika baadhi ya shule. Pia, utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa wa sekondari ngazi ya juu ulioahirishwa kuanza Julai mwaka 2024, utaanza na kidato cha tano Julai mwaka huu.

Waraka huo unaeeleza kuwa mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya stashahada mwaka wa kwanza yataendelea kutumia mtaala ulioboreshwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button