WASICHANA 6,685 wenye umri kati ya miaka 13 na 21 waliokatisha masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali ukiwemo ujauzito wamejisajili kuendelea na masomo kwa njia mbadala chini ya Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP- AEP).
Wasichana ahao wamesajiliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wake ulipoanza rasmi mwaka 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dk Michael Ng’umbi amesema hayo Machi 2, 2023 mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa Baraza la 13 Wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Dk Ng’umbi amesema mradi huo unaotekelezwa na Taasisi hiyo ulianza mwaka jana (2022) na ulisajili wasichana 3,333 walianza masomo hayo na wanaendelea na masomo katika vituo mbalimbali vya taasisi hiyo nchini.
Mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo amesema kwa mwaka wa masomo wa 2023 na hadi kufikia Februari mwishoni wasichana 3,352 tayari wamejisajili kuendelea na masomo yao.
“ Tumepata mafanikio makubwa tangu kuanza kwa mradi kwani katika kipindi cha mwaka jana (2022 ) kwa kuvuka lengo kwa kuwasajili wasichana 3,333 ambao wanaendelea na masomo yao ” amesema Dk Ng’umbi
Dk Ng’umbi amesema mradi huo unalenga kunufaisha wasichana 12, 000 nchini ambapo kila mwaka utasajili wanafunzi 3,000 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2022 hadi kufikia mwaka 2026 .
Mradi huo unalenga kuwapatia elimu ya sekondari bila malipo wasichana waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari kwa sababu mbali mbali ikiwemo kupata ujauzito au hali ngumu ya maisha.
Dk Ng’umbi ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kugharamia ujenzi wa Hosteli , na kutoa chakula kwa wasichana hao ili kiwe kichocheo cha kuudhuria masomo hayo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan iliwaondolea vikwazo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito.
Mradi huo unatekelezwa na taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TEMISEMI) kwa ufadhili wa Benki Dunia.