Wasikilizaji Ebony FM wawasaidia mil 10.9/- walemavu Njombe

KIKUNDI cha Team Thamani kilichoundwa na wasikilizaji zaidi ya 700 wa vipindi vya mtangazaji Eddo Bashir wa redio Ebony FM ya Iringa, kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi walemavu 80 wa Shule ya Msingi Mchanganyiko ya Kibena, mjini Njombe.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 10.9 unajumuisha vyakula mbalimbali, baiskeli za walemavu, magodoro na mashuka, mashine za kufulia nguo, pamoja na zawadi nyingine, ikiwa ni juhudi za kikundi hicho kusaidia watoto hao wenye mahitaji maalumu shuleni hapo.

Bashir, ambaye pia ni mratibu wa kikundi hicho, alisema kila mwanachama wa Team Thamani alichangia Sh 15,000 kufanikisha mradi huo.

“Hawa ni wasikilizaji wa vipindi vyangu kutoka maeneo mbalimbali nchini ambako Ebony FM inasikika. Kwa pamoja tumeweza kuchangisha zaidi ya Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya watoto hawa,” alisema Bashir.

Alifafanua kuwa kikundi hicho kimekuwepo kwa zaidi ya miezi saba na tayari kimewahi kusaidia jamii nyingine zenye uhitaji katika vijiji vya Image na Pomerin, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.

Kwa pamoja, wanachama 700 wa Team Thamani walisafiri hadi Njombe kushiriki tukio hilo, jambo ambalo Bashir alisema limeleta hamasa kubwa.

“Nashukuru sana kwa juhudi za wanachama. Hili ni jambo kubwa na la kumshukuru Mungu,” aliongeza.

Alisema Team Thamani  itaendelea kutoa msaada kwa jamii kila baada ya miezi mitatu, kwa lengo la kuwasaidia wasiojiweza na kuleta mabadiliko chanya.

Mwalimu wa wanafunzi walemavu, Patrick Job, alisema msaada huo utaboresha maisha ya watoto hao wenye changamoto mbalimbali, zikiwemo ulemavu wa viungo, albino, akili, uwezo wa kuona na kuongea.

“Msaada wa magodoro na baiskeli utatatua changamoto kwa asilimia 100,” alisema akizungumzia ukubwa wa msaada huo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo  Frolence Bujeni, alisema msaada huo ni hatua kubwa, lakini bado kuna mahitaji ya kila siku yanayohitaji msaada wa wadau.

“Team Thamani imesaidia kupunguza changamoto za watoto hawa. Tunaomba wadau waendelee kutuunga mkonohasa kwa mahitaji ya kila siku ya wanafunzi hawa,” alisema Bujeni.

Shule ya Msingi Mchanganyiko ya Kibena ina jumla ya wanafunzi 960, wakiwemo wanafunzi 80 wenye mahitaji maalumu, ambao wanategemea msaada wa jamii ili kufanikisha ndoto zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button