Wasiopeleka watoto shule kusakwa nyumba kwa nyumba

MKUU wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa, amesema atafanya msako wa nyumba kwa nyumba, ili kubaini wazazi ambao wameshindwa kuandikisha watoto wao shule.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ziara yake ya kukagua maandalizi ya upokeaji wa wanafunzi wa madarasa ya awali,shule ya msingi pamoja na kidato cha kwanza katika shule zilizopo wilayani kwake.

Amesema haiwezekani serikali itoe fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu sambamba na elimu bure, huku wazazi na kwa makusudi wanashindwa kuwapeleka shule watoto wao.

“Kwa hili tusilaumiane wazazi na walezi, naanza msako wa nyumba hadi nyumba Jumatatu na nikikuta mtoto ambaye anatakiwa awepo shule kisha yupo nyumbani atapambana na hatua kali za kisheria,” amesema DC Mgandilwa.

Jiji la Tanga mpaka Sasa limeandikisha asilimia 51 pekee ya watoto wa darasa la awali na la kwanza huku kwa upande wa sekondari wakifikia asilimia 61.

Habari Zifananazo

Back to top button