Wasira: Hakuna makundi CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kipo shwari na hakuna makundi ndani ya chama hicho.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira alieleza hayo katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV juzi usiku.

Wasira alisema nguvu ya CCM ipo katika umoja kwa kuwa umoja ni nguvu na huleta ushindi.

“CCM ni chama kikubwa tuna wanachama wengi milioni 13 lakini pamoja na wingi wetu hali ya siasa ndani ya chama ni shwari tuna umoja wa kutosha na tunaamini umoja ni nguvu,” alisema.

Aliongeza: “Ndani ya CCM hakuna makundi lakini kwa wanaogombea kunakuwa na makundi ya muda uchaguzi ukiisha na yenyewe yanaisha lakini CCM kama chama hakuna makundi”.

Wasira alisema hali ya kisiasa nchini ni nzuri lakini manung’uniko yapo kwa sababu hakuna nchi isiyokuwa na manung’uniko au kuridhika na kila kitu.

“Tangu nilipokuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM nimesafiri katika mikoa 13, ni nusu ya Tanzania kama ningekuwa mtaalamu wa takwimu ningeeleza kwa sampuli niliyonayo hali ya siasa ni nzuri… hakuna nchi unayoweza kusema haina mtu ananung’unika hata ufanyaje,” alisema.

Wasira alisema manung’uniko ya watu yanaiwezesha serikali kujua matatizo ya wananchi na kuyafanyia kazi kwa sababu hakuna nchi isiyokuwa na matatizo.

Alisema Tanzania imepitia nyakati ngumu wakati wa kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli lakini CCM iliendelea kusimamia majukumu yake ya msingi ya kusimamia umoja wa kitaifa na hata wakati wa janga la Covid 19 serikali ilihakikisha uchumi unarudi katika hali himilivu.

Wasira alisema wanachama wa CCM kwa sasa wanasajiliwa kupitia mifumo ya kidijiti na mpaka sasa wana wanachama milioni 13 na wanaendelea kusajili wanachama wasioingia katika mifumo

Alisema serikali ilisikiliza maoni ya vyama vya siasa na kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi hivyo madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu mabadiliko ya sheria kuelekea uchaguzi hayana mashiko na haiwezi kuahirisha uchaguzi kwa sababu uchaguzi upo kikatiba.

Wasira alisema madai hayo ya mabadiliko ya sheria yanayotolewa na Chadema hayainyimi usingizi CCM kwa sababu si rahisi kuwa na mfumo mmoja unaowaridhisha watu wote kwa wakati mmoja.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button