Wasomi watia neno uchumi miaka 63 ya uhuru

SERIKALI imeshauriwa kutumia vizuri rasilimaliwatu ili kuendelea kuimarisha uchumi.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Profesa Haji Semboja alisema ili kuwe na maendeleo ya kiuchumi yatakayosaidia kupunguza umasikini ni lazima taifa liajiri watu kutokana na mifumo rasmi ya ajira.
Profesa Semboja alisema mifumo rasmi ya ajira inazingatia ushindani wa ajira sokoni na yenye uwazi inayozingatia uwezo wa mtu, elimu ya mtu na fani kulingana na kazi inayotangazwa na si kuajiri kwa kuangaliana sura na kuingiza undugu na urafiki katika kazi.
“Nafasi zitangazwe kwa uwazi kabisa, watu washindane kwa uwezo na elimu zao na mwisho mshindi apatikane na aonekane kweli amewashinda washindani wake kwa haki, nina uhakika nchi itasonga mbele kiuchumi kwa haraka sana kwa sababu ataweza kumshauri rais kwa umakini na weledi mkubwa,” alisema.
Profesa Semboja alisema ikiwa mifumo ya ajira haitaachwa huru ifanye kazi zake, watu watapewa nafasi kwa uchawa wao na mwisho hawataweza kumsaidia rais na nchi haitapiga hatua na badala yake itabaki palepale au itarudi nyuma.
Naye Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Profesa Humphrey Moshi alisema kwa sasa kuna maendeleo makubwa ya kiuchumi ikilinganishwa na miaka ya mwanzo ya kujitawala kutokana na ongezeko la watu na kushauri kuimarisha sera na sheria za uwekezaji zinazoendana na wakati.
“Nchi inakwenda vizuri, kinachotakiwa kwa sasa ni kuimarisha mifumo ya kisheria na sera ziendane na wakati wa sasa pamoja na matakwa ya nchi,” alisema Professa Moshi.
Alisema serikali inapaswa iangalie namna bora ya kuimarisha sarafu ya Shilingi kwa sababu jinsi Shilingi inavyozidi kushuka thamani ikilinganishwa na Dola ya Marekani, ndivyo maisha yanavyozidi kuwa magumu hivyo ni vema serikali ikatilia mkazo sekta za madini, utalii na viwanda ili kuimarisha sekta ya fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa uchumi na Biashara, Gabriel Mwang’onda alisema Tanzania imeimarika zaidi katika eneo la kijamii kama vile afya, elimu, maji, miundombinu, usafiri na usafirishaji pamoja na viwanda ikilinganishwa na miaka 63 iliyopita.
Alisema miaka ya 1960 taifa lilitegemea kilimo kama nguzo kuu ya uchumi lakini baada ya miaka 63 leo hii taifa linategemea sekta zote ili kujenga ustawi wa Watanzania kama vile sekta za viwanda, kilimo, uzalishaji, biashara, uwekezaji, utalii, ufugaji na uvuvi



