DAR-ES-SALAAM : WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kutoa motisha na kuwajengea uwezo wataalam ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanavyojitokeza duniani kwa lengo la kuendelea kuimarisha utoaji wa matibabu nchini .
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila amesema serikali itasimamia ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma bora za afya popote alipo na kwa wakati.
Aidha ameupongeza uongozi na watumishi wa Muhimbili kwa namna wanavyotoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wananchi kwa kuzingatia weledi ubora unaotakiwa.
“Sekta ya afya hapa Tanzania ndani ya miaka hii mitatu imekuwa kuliko kipindi chochote kwani katika hospitali zetu za Taifa na kipekee Muhimbili tunazo zaidi ya aina 35 za matibabu ya ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa uloto, upandikizaji wa figo, matibabu ya magonjwa ya moyo, uwekezaji ambao unaacha deni kwetu la kutoa huduma bora kwa Watanzania wenzetu ili waweze kufurahia matunda ya uwekezaji huo” amebainisha Mhagama
Mhagama amesema serikali imejenga miundombinu, kuna vifaa tiba vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu na kusomesha wataalam na imewezesha wataalam hao kutoa huduma za ubingwa bobezi na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa matibabu.
SOMA : Idara ya kinga mjipange usafi wa majiji
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Dk Ellen Senkoro amemuhakikishia kuwa bodi hiyo itashirikiana na menejimenti kuhakikisha kuwa wanatafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia na maelekezo ya wizara.
“Hatimaye watu wote wanaotibiwa Muhimbili wapate huduma bora na zenye kukidhi matarajio yao.