” Wataalamu watasaidia kutatua changamoto”

WAHITIMU wa Chuo cha Ustawi wa Jamii wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuwa fursa ya ajira.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 48 ya chuo hicho mapema hii leo, Waziri wa Maendelo ya Jamii Jinsia Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima leo amesema wahitimu waende wakaitumikie jamii kwa kile walichojifunza nasio kupoteza taaluma zao.

“Nimewaambia wahitimu wote hii isiwe safari ya mwisho ya kusoma mnatakiwa kujiendeleza kimasomo, bila kuwa wabinafsi bali kujitoa kwa maendeleo ya jamii, kwa kuwa tunahitaji wasomi zaidi na bado tunahitaji mafanikio kwenye kada hii muhimu katika jamii,”

Advertisement

“Kutokana na ukweli kwamba nafasi za ajira katika sekta ya umma ni chache, tumieni utaalamu mliopata ili kujitafutia ajira binafsi na kuajiri wengine. Napenda kuwakumbusha kudumisha uzalendo, utii na maadili ufanya hivyo mtaweza kuisaidia jamii na taifa letu kwa ujumla,” amesema  Gwajima

Gwajima amesema serikali ipo kimkakati katika kuhakikisha kada ya ustawi wa jamii inakuwa ni kada iliyojitosheleza na inajibu mahitaji ya nchi katika kipindi hiki cha maendeleo ya kidigitali.

“Tunaona wazazi na walezi wapo bize kukimbizana na uchumi hivyo lazima serikali ijue watoto na familia zao zinakuwa vipi katika masuala ya ustawi,”amesema.

Alibainisha kuwa kutokana na hilo serikali inaanda Sheria ya huduma ya ustawi wa jamii ili wahitimu wa kada hiyo wakishafunzu wawe na msajili wao anayewapa  leseni za kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yatokanayo na taaluma zao.

“Tukifanya hivyo tutaongeza wigo wa wahitimu kwenda kujiajili wenyewe aidha kwa kufungua vituo vyao binafsi vya kutoa huduma za ustawi wa jamii kama ilivyo kwenye sekta za huduma ya afya na elimu,” alisema.

“Hongereni pia kwa kuanzisha mitaala mipya inayolenga kuzalisha wataalamu katika fani za kazi za Jamii, Watoto na Vijana, Masoko na Ujasiriamali, Utatuzi Mbadala wa Migogoro Mahala pa Kazi na Saikolojia.

“Ni wito wangu kwa chuo kuendelea kuwa wabunifu ili kuendana na mahitaji ya wakati na soko. Ni imani wataalamu wanaotokana na mitaala hii mipya, watasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii yetu katika kipindi hiki cha utandawazi,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Dk Joyce Nyoni alieleza kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa, uhaba wa mabweni, ufinyi wa bajeti pamoja na kumbi za mikutano ya mihadhara.

“Chuo kinatumia bajeti ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi mmoja wa mihadhara unaoendelea. Chuo kinapenda kujenga kumbi zingine za mihadhara, lakini ufinyu wa bajeti umekuwa ni changamoto kubwa, tutaendelea kuiomba Wizara hiyo iwasaidie kupata fungu zaidi kutoka Serikalini na wafadhili ili kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia,”amesema Nyoni

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa chuo hicho, Sophia Simba alisema mwelekeo wa chuo ni kuendelea kutekeleza dira ya nchi kwa vitendo na weledi wa hali ya juu katika kutoa mafunzo, kufanya utafiti, na kutoa ushauri elekezi kulingana na mahitaji ya jamii na taifa kwa ujumla.

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 3121 ambao  asilimia 65.5 ni wanawake na asilimia 34.6 ni wanaume  watatunikiwa vyeti vyao  katika fani za mbalimbali za ustawi wa jamii ikiwemo  kazi za jamii kwa vijana na watoto, makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto, mahusiano kazini na menejimenti ya sekta ya umma, menejimenti ya rasilimali watu pamoja  na uongozi wa biashara.