Watakaowahi tutakunywa nao chai – JWTZ

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa siku saba kuanzi leo August 24,2023 kwa Wananchi kusalimisha mavazi ya Jeshi au yanayofanana na sare za Jeshi ambapo baada ya siku saba Wanajeshi watakuwa mtaani kukusanya mavazi hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu JWTZ Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amesema wametoa siku saba kuanzia leo iwe mwisho wa kuyavaa, kuyatumia au kuyauza.

” Kwa wale wasanii, watafuata utaratibu wa kuomba kibali ili waruhusiwe kutumia mavazi hayo, baada ya siku saba atakayekutwa na mavazi hayo atachukuliwa hatua kali ambayo itakuwa fundisho kwa wengine. ” Amesema na kuongeza

“Mavazi yawasilishwe kwenye makambi ya Jeshi, Vituo vya Polisi au kwa Wajumbe wa Serikali za Mitaa, hatutokuuliza umeipata wapi na ukifika wakati wa chai tutakunywa nae chai pamoja, tunatoa siku saba kuyasalimisha. ” Amesisitiza

Ilonda amesema mtu ambae hatosalimisha atakuwa na nia ovu na dhamira mbaya na atakuwa na lake jambo.

” Waswahili wanasema Mwanakulitafuta Mwanakulipata, kwahiyo Mwanakulitafuta baada ya siku saba atakuwa Mwanakulipata. “Amesema

Amesema, zipo baadhi ya Taasisi zinazowashonea Watumishi sare za aina hiyo, wapo pia Wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia katika maduka au maeneo yao ya biashara, wapo baadhi ya Wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu.

“Baadhi ya Watu wanatumia mavazi hayo kuwatapeli Wananchi kwa kujifanya Wanajeshi na wengine kufanya vitendo viovu huku wakidhaniwa kuwa ni wanajeshi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi na hakipaswi kufumbiwa macho.”Amesema

Amesema, katazo hilo ni kwa mujibu wa kufungua cha 99 cha Sheria ya Usalama wa Taifa sura ya 192, sheria namba 24 ya mwaka 1966.

.

Habari Zifananazo

Back to top button