Watakiwa kuwa mabalozi sheria za madini

SHINYANGA: Serikali imewataka wakaguzi wakuu wa migodi na mameneja wa migodi nchini kuwa mabalozi wa utekelezaji wa sheria, kanuni za madini na kuwa wazalendo katika biashara ya madini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa leo Aprili 24, 2026 wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na mtaalamu kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini Tume ya Madini, Mhandisi Erasmina Massawe, kwenye mafunzo kwa mameneja na Wakaguzi Wakuu wa Migodi ya uchimbaji mdogo yaliyowakutanisha washiriki kutoka mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga.

Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uelewa wa kitaalam, usimamizi bora wa migodi, uzingatiaji wa sheria na kanuni za madini pamoja na kukuza uchimbaji salama na endelevu.
Amesema mbali na kujifunza mbinu za kuimarisha usalama migodini, viongozi hao wanapaswa kuwa sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuhakikisha biashara ya madini inafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia Sheria ya Madini na kanuni zake, hatua itakayosaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini, ikiwemo uboreshaji wa mfumo wa biashara ya madini, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, uwepo wa maafisa migodi wakazi katika maeneo ya uchimbaji pamoja na ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliosaidia kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Aidha, amesema Serikali imeimarisha ulinzi na ufuatiliaji wa madini kwa kuweka wakaguzi katika maeneo muhimu kama viwanja vya ndege, bandari, mipakani na katika maeneo yote ya uzalishaji madini, sambamba na kusimamia utoaji wa vibali vya usafirishaji wa madini na utekelezaji wa sheria ya kodi ikiwemo ondoleo la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye baadhi ya shughuli za madini.

Akizungumzia uwezeshaji wa Watanzania kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo, Mhandisi Massawe amesema maboresho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini yameongeza kwa kiasi kikubwa ushiriki wa watanzania katika usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali migodini.
“Kwa sasa zipo fursa nyingi katika Sekta ya Madini ikiwemo huduma za chakula, ulinzi, vifaa kinga, huduma za kisheria, ujenzi na bima. Watanzania wanapaswa kuzitumia fursa hizi kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa nchi,” amesisitiza.
Wakati huohuo amehimiza wadau wa madini nchini kutumia maabara bora ya Tume ya Madini iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupimiwa madini yao na sampluli za madini ili kufanya biashara ya madini ya uhakika.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi wa uchimbaji mdogo na kuhakikisha rasilimali za madini zinaleta manufaa mapana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.



