Watakiwa kuwashirikisha wadau uchaguzi mdogo

WATENDAJI wa uchaguzi kwenye uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara wametakiwa kuwashirikisha kwa ukaribu wadau wa uchaguzi kwenye maeneo yao.

Pia wametakiwa kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele alitoa wito huo Februari 20, 2024  wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayofanyika Morogoro.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  hivi karibuni ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo  katika  kata hizo  Machi 20, 2024 ambapo fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia  Februari 27, 2024 hadi Machi 4, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 4, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Machi 5 hadi 19, 2024.

“Napenda niwakumbushe na kuwasisitiza kuwa, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi , ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia  utekelezaji wa majukumu yenu,” alisema  Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele pia aliwakumbusha  juu ya umuhimu wa kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala.

Alisema ni muhimu kwa watendaji hao wa uchaguzi, kuhakikisha wanayatambua na kuyajua  vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.

Jaji Mwambegele alisisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya utambuzi na kukagua  vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la  kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

“Tuachane na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi,” alisema  Jaji Mwambegele.

“Mhakikishe siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo utahitajika ushauri kuhusiana na masuala ya uchaguzi,” Jaji Mwambegele aliwasisitiza watendaji hao.

Hivyo aliwakumbusha  kuwa uchaguzi ni jambo la kisheria na kwamba sheria na taratibu zikifuatwa ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa  uchaguzi, mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Hata kama umeshasimamia chaguzi kadhaa hapo nyuma, lakini uchaguzi huu mdogo unaojumuisha kata 23 haujawahi kuusimamia,” alisema Jaji Mwambegele.

Habari Zifananazo

Back to top button