Watakiwa kuweka mikakati uzalishaji mbegu bora za mihogo

WATAFITI wa Mazao Jamii ya Mihogo na Viazi kutoja Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kituo cha Naliendele wamewataka watendaji wa Halmashauri mikoa ya Kusini kuweka mikakati endelevu ya kuwekeza katika utumiaji wa mbegu bora za Mihogo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hili nchini.
Akiongea Mkoani hapa ,mmoja wa watafiti hao Festo Masisila amesema hatua hizo ni pamoja na Halmshauri kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mbegu bora za Mihogo ambazo zimethibitishwa na kuidhinisha na Mamlaka husika kwa ajili ya Kilimo ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.
“Kuna mbegu zaidi ya nane ambazo zimethibitishwa na kuidhinishwa na Taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu nchini (TOSCI) na uzalishaji wake ulianza mwaka 2022 na zimeanza kutumika,” amesema.
Masisila alitaja mbegu hizo kuwa ni TARICASSA 1, 2, 3, 4, na 5, aina nyingine ni Mkuranga, Chereko Kiroba, Kipusa na Mkumba.
Amesema mbegu hizo zina uwezo wa kuzaa mara tatu zaidi kulinganisha na mbegu za asili ambazo wakulima wanalima kwa wingi sana.
“Mbegu hizi bora mbegu ya chini kabisa inazaa tani 22 kwa hekari mbili lakin mbegu ya asili inazaa tani 8 kwenye hekari 2.5,” amesema.
Amesema wakulima wakitumia mbegu bora ambazo zimeidhinishwa itasaidia kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani nane kwa hekari 2.5 nusu itasaidia kuongeza uzalishaji mpaka wastani wa tani 24 kwa hekari 2.5.
Amesema kuna baadhi ya mbegu hizo bora ambazo zinazaa mpaka tani 50 Kwa hekari 2.5, zingine tani 40, 39, na 30.
Masisila amesema hayo wakati wa zoezi la kufanya tathmini ya ubora zaidi wa mbegu hizo ambazo zilipandwa kupitia shamba darasa kwa wakulima wa mihogo kata ya Mkunwa Halmashauri ya Mtwara Mkoani Mtwara.
Amesema mbegu hizo ni bora na kwamba kila moja ina sifa yake ikiwemo kukomaa haraka, kuzaa kwa wingi, kuhimili magonjwa.
Katika hatua nyingine wakulima hao wameishukuru TARI Naliendele kwa kuanzisha shamba darasa katika maeneo yao na kuwashirikisha katika kutafiti mbegu bora zaidi kati ya hizo Zaid ya nane.
“Kwanza kabisa sisi wakulima tumapata fursa ya kujifunza Kwa uhalisia kabisa kuhusu ubora wa hizo mbegu ambazo zimethibitishwa kuwa ni bora, na tumeweza kujua namna bora ya upandaji wa hizo mbegu na sasa tunaenda kuzitumia ili tuongeze uzalishaji,” amesema Fatma Ally Mkulima wa Mihogo Kata ya Mkunwa Halmashauri ya Mtwara.