Watanzania kunufaika uwekezaji kidigitali

WATANZANIA watanufaika na fursa za uwekezaji kupitia mfuko wa Sanlam Pesa Money unaolenga kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuwapa njia rahisi ya kukuza mitaji yao kupitia mifumo ya kidijitali.
Unufaikaji huo umetokana na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Sanlam Investments East Africa Limited (SIEAL) kuingia mkataba endelevu.
Vijana, wanawake, wafanyabiashara na wakazi wa vijijini, watawekeza kwa kiwango cha chini cha Sh 10,000 pekee. Hii inawapa nafasi hata wale wenye kipato cha kawaida kuanza safari ya uwekezaji bila mtaji mkubwa.
Kwa kutumia matawi ya CRDB, wakala wa benki hiyo pamoja na mifumo yake ya kidijitali kama SimBanking, wananchi watapata fursa ya kuwekeza kwa njia rahisi na salama hatua itakayoondoa vikwazo vya baadhi ya watu kushindwa kuwekeza kutokana na ugumu wa kupata huduma hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema kuwa ushirikiano huo utaongeza fursa kwa Watanzania kujifunza kuhusu uwekezaji na kuweka akiba kwa manufaa ya baadaye.

“Benki ya CRDB imejikita katika kuwawezesha wananchi kifedha kwa kuhakikisha wanapata suluhisho rahisi za uwekezaji. Ushirikiano huu unaleta mapinduzi makubwa kwa kuwa unarahisisha mchakato wa uwekezaji kupitia mifumo yetu ya benki na kidijitali,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Investments East Africa, Jonathan Stichbury, amesema kuwa mfuko wa Sanlam Pesa Money Market Fund unatoa nafasi kwa kila Mtanzania kupata faida kutokana na akiba yao huku wakihakikishiwa usalama wa mtaji wao.



